Pinda Afungua Mkutano wa Majaji wa Haki za Binadamu Afrika

Waziri Mkuu , Mizengo Pinda akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa Majaji wa Afrika uliofanyika kwenye Hoteli ya Ngurdoto, Arusha Novemba 4.

Waziri Mkuu , Mizengo Pinda akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa Majaji wa Afrika uliofanyika kwenye Hoteli ya Ngurdoto, Arusha Novemba 4.

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema Serikali ya Tanzania imepania kuboresha upatikanaji wa haki kwa raia kwa kusogeza huduma za mahakama karibu na wananchi.

“Tumeusaidia mhimili wa mahakama katika nia yake ya kujenga Mahakama Kuu katika kila mkoa na Mahakama ya Hakimu Mkazi katika kila wilaya. Uwepo wa mahakama hizi utasaidia kuhakikisha kuwa haki inapatikana kuanzia kwenye mahakama za chini hadi za juu.”

Ametoa kauli hiyo Novemba 4, 2015 wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Majaji wa Haki za Binadamu barani Afrika ulioanza leo jijini Arusha. Akifungua mkutano huo wa siku tatu kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu alisema ili kuboresha zoezi hilo, hadi sasa Mahakama Kuu zimeshajengwa kwenye mikoa 14 kati ya 26 ya Tanzania Bara.

Alisema mkutano huo unazihusu mahakama maalum zinazohusika na masuala ya utoaji wa haki za binadamu na ziko tofauti na mahakama za makosa ya jinai (kama wizi, kuua, n.k.)

“Katika nchi nyingi za Afrika, asilimia kubwa ya wananchi wake wanakosa uhuru wa kutumia mahakama za aina hii na tumesikia kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi saba tu zilizoridhia kusaini mkataba wa kuanzishwa kwa mahakama hizo.”

“Tanzania imeenda mbali, mahakama hii ipo hapa Arusha na Rais wake ni Jaji Mkuu Mstaafu, Jaji Agustino Ramadhani. Hapa nchini mtu ambaye alikuwa akiitumia sana mahakama hii ni marehemu mchungaji Christopher Mtikila. Yeye akiwa na jambo analoamini haki haikutendeka, kila mara alitumia uhuru huo na kufungua kesi kwenye hiyo mahakama,” alisema.

Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu alisema ili kuhakikisha mhimili wa mahakama unajitegemea kifedha, Serikali ilianzisha Mfuko wa Mahakama (Judiciary Fund) chini ya Sheria namba 4 ya Utawala wa Mahakama ya mwaka 2011. “Tangu mwaka 2012/2013, fedha za mfuko huu zimeongezeka kutoka sh. bilioni 57.8 na kufikia sh, bilioni 89.6 katika mwaka 2014/2015 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 54.8,” alisema.

Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa mkutano huo, Rais wa Mahakama ya Haki za Binadamu barani Afrika, Jaji Agustino Ramadhani alisema nchi 29 kati ya 54 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) zilikubali mfumo wa mahakamo hizo ufanye kazi nchini mwao lakini ni nchi saba tu ambazo zimekubali kusaini mkataba wa kuanzishwa kwa mahakama hizo.

Alizitaja nchi hizo kuwa ni Burkina Faso, Ghana, Mali, Malawi, Cote d’ Ivoire, Rwanda na Tanzania. Alitoa wito kwa nchi nyingine wanachama wa AU kuharakisha utiaji saini wa mkataba huo.