Pinda Aalika Wawekezaji Sekta za Afya, Kilimo na Nishati
*Obasanjo asisitiza ajira kwa vijana Afrika
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali imefungua milango kwa wawekezaji kwenye sekta zote lakini mkazi unaelekezwa zaidi kwenye sekta ya afya, kilimo hasa usindikaji mazao, nishati na miundombinu. Ametoa kauli hiyo Oktoba 20, 2014 wakati akishiriki Mjadala wa Marais (Presidential Keynote Panel) kuhusu fursa za uwekezaji barani Afrika uliolenga kuonyesha fursa za uwekezaji zilizopo barani Afrika hasa katika nchi za Tanzania, Uganda, Ghana na Rwanda ambao umeanza leo kwenye hoteli ya Savoy, jijini London, Uingereza.
Waziri Mkuu aliwasili jijini London jana mchana kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi unaohusu uwekezaji barani Afrika (The Global African Investment Summit – TGAIS) kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete na ameshiriki mjadala huo pamoja na Rais John D. Mahama wa Ghana, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda.
“Tunahitaji wawekezaji kwenye sekta nyingi lakini zaidi kwenye sekta ya afya katika vyuo vya tiba na uuguzi ili tupate watumishi wa kutosha, utengenezaji wa madawa na vifaa vya hospitali na ujenzi wa hospitali,” alisema.
Aliyataja maeneo mengine ya kipaumbele kuwa ni kilimo na na hasa usindikaji wa mazao, hasa ikizingatiwa kwamba asilimia kubwa ya Watanzania inategemea kilimo kwa kujikimu. “Watanzania wengi bado wanategemea kilimo kama njia yao kuu ya uzalishaji, tunahitaji pia kupata umeme wa kuendesha viwanda kutokana na gesi, makaa ya mawe pamoja na geo-thermal,” aliongeza.
Akizungumzia kuhusu uwekezaji kwenye miundombinu, Waziri Mkuu alieleza Serikali ilivyojipanga kujenga reli mpya yenye urefu zaidi ya km. 2,000 kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, reli ya kutoka Tanga kupitia Arusha hadi Mwanza na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo pamoja na uimarishaji wa bandari za Tanga, Mtwara na Dar es Salaam.
Kwa upande wao, Marais wa Ghana, Uganda na Rwanda walielezea fursa zilizopo nchini mwao kwenye maeneo ya madini, miundombinu ya barabara na reli, umeme, na teknolojia ya habari na mawasiliano.
Mapema, akiwakaribisha wajumbe wa mkutano huo wa siku mbili, Mwenyekiti wa mkutano huo, Rais mstaafu wa Nigeria, Bw. Olesegun Obasanjo alisema bara la Afrika lina nafasi kubwa ya kuendeleza sekta za maenedeleo kupitia uwekezaji maliasili, Kilimo na usindikaji mazao, nishati na utalii.
“Nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara zina fursa nyingi za uwekezaji na siyo hizi nne ambazo zimewakilishwa leo hapa za Tanzania, Uganda, Ghana na Rwanda. Kuna miradi yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 200 ambayo itapata fursa za kunadiwa kwa wawekezaji kupitia mkutano huu,” alisema.
“Nimewaalika Marais kutoka nchi hizi nne ili watupe mwanga wa kile tunacheweza kufanya katika nchi zao… lakini vilevile tutambue katika bara la Afrika kuna vijana wengi ambao ni zaidi ya asilimia 60 ambao hawana kazi. Tutakuwa tumepotoka tusipoliangalia kundi hili. Ni lazima miradi inayotafutiwa wawekezaji ilenge kuleta ajira kwa vijana wetu, wapate kipato (wealth creation) na technology transfer,” alisema.
Mkutano huo unahudhuriwa na wakuu wa makampuni na taasisi za kibiashara zaidi 400.