Refarii mmoja nchini Ujerumani alishangaza wengi baada yake kuondoka uwanjani na kuacha mechi imesimama kufuatia kisa kilichomhusisha meneja wa timu moja iliyokuwa ikicheza uwanjani.
Refa Felix Zwayer aliondoka baada ya meneja wa Bayer Leverkusen Roger Schmidt kukataa kutii amri yake ya kumtaka aondoke uwanjani kwa kosa la kulalamika sana.
Mechi hiyo ya Bundesliga dhidi ya Borussia Dortmund ilicheleweshwa kwa dakika nane hivi na ilirejelewa baada ya Schmidt mwishowe kukubali kuondoka eneo la kiufundi.
Schmidt alikuwa amedai kuwa bao la Dortmund, lililofungwa na Pierre-Emerick Aubameyang, halikufaa kukubaliwa.
Mkufunzi huyo wa umri wa miaka 48 alisema mkwaju wa adhabu uliopelekea kufungwa kwa bao hilo haukupigiwa eneo sahihi.
Kutokana na kulalamika kwake, alifukuwa eneo la kiufundi, lakini akakataa kubanduka.
Refa Mjerumani Zwayer alimsihi kaimu nahodha wa Leverkusen Stefan Kiessling, aliyekuwa amefanya madhambi yaliyosababisha mkwaju huo wa adhabu, amsihi meneja wake aondoke.
Baada ya hilo kushindikana, Zwayer aliondoka uwanjani na kuingia chumba cha kubadilishia mavazi. Alifuatwa na wachezaji.