Pembejeo za Ruzuku Bomba la Ubadhirifu – Zitto Kabwe

Zitto Kabwe

Zitto Kabwe

Na Zitto Kabwe

MKULIMA wa mahindi anayelima hekta moja anahitaji mbegu na mbolea za kupandia na kukuzia zenye thamani ya tshs 220,000. Kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula nchini Serikali iliamua kuanzisha mfumo wa kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima wa hali ya chini. Kwa mfumo huu serikali hulipia tshs 140,000 kupitia vocha anazopewa mkulima na kuziwasilisha kwa mawakala wa mbolea na mbegu. Hivyo mkulima hulipia tshs 80,000 tu.

Serikali kupitia wizara ya kilimo na chakula hutengeneza Vocha hizo na kuzigawa mikoani ambapo napo huzigawa wilayani kisha vijijini. Serikali ya Kijiji kupitia mkutano Mkuu wa kijiji huteua wafaidika wa mfumo huu na kuwapa Vocha. Wao hupeleka Vocha hizi kwa mawakala wa pembejeo, wanalipa fedha ya juu na kupewa mbolea na mbegu. Mawakala hupeleka fedha hizi Benki ya NMB ambayo huwalipa mawakala fedha ya thamani ya Vocha.

Wizara ya Fedha nayo huilipa NMB ambayo hutoa huduma hii kwa riba ya 4%. Mwaka 2012/13 jumla ya wakulima 2m walifikiwa kwa mujibu wa taarifa ya Serikali. Kwa ujumla toka mwaka 2008/09 mpaka 2013/14 Serikali imetumia jumla ya tshs 574 bilioni katika mradi huu. Sehemu ya fedha hizi ni mkopo wa benki ya Dunia wa dola 160m.

Habari hii ikiishia hapa ni habari Njema sana na yenye malengo mazuri kabisa ya kujenga uwezo wa wananchi kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na kuondoa umasikini nchini. Wastani wa tshs 93 bilioni kwenda kwa wananchi wa vijijini ni mfumo bora kabisa wa dola kujengea uwezo wananchi wake. Hata hivyo jambo jema limegeuka moja ya skandali kubwa sana katika historia ya nchi yetu.

Kwanza mradi umegubikwa na changamoto zisizokwisha za uteuzi mbovu wa mawakala wa pembejeo, uteuzi mbovu na wa upendeleo wa wafaidika wa mradi, ucheleweshaji mkubwa wa pembejeo kufika na wakati mwingine kufika wakati msimu wa kupanda umepita na mwisho wananchi kupewa mbolea bandia na hata mbegu zenye ubora hafifu.

Pili, mfumo mzima umegundulika ni wa kifisadi ambapo orodha ya wafaidika huchakachuliwa kiasi cha kuweka hata watu waliokufa kwamba wamepokea mbolea. Kamati ya Bunge ya PAC katika kikao chake na wizara ya kilimo na mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali tarehe 28 January 2014, iliambiwa kuwa baadhi ya maeneo nchini mawakala walikuwa wananunua Vocha kutoka kwa wakulima kwa tshs 10,000. Katika jimbo la uchaguzi la kigoma kaskazini mawakala walinunua Vocha hata kwa shs 2000 na wao kwenda kulipwa tshs 140,000 huko benki kana kwamba waliuza mbolea ile kwa wakulima.

Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia katika mkoa wa kilimanjaro mwaka 2012 uligundua kuwa asilimia 60 ya pembejeo zilichukuliwa na viongozi wa serikali za vijiji. Kiuhakika, nchi nzima viongozi wa vijiji wanatuhumiwa kuiba Vocha na kushirikiana na mawakala kujipatia fedha kwa njia za kifisadi.

Inasemekana kuwa asilimia kati ya 60 na 70 ya Bajeti ya pembejeo ya ruzuku haikufikia walengwa na ilitafunwa na mtandao wa maafisa wa wizara ya kilimo, wakuu wa wilaya na makampuni ya mbolea na mawakala wa pembejeo Kamati ya PAC imeagiza CAG kufanya uchunguzi wa kiforensiki (forensic investigation) ili kuweza kubaini wabadhirifu wa mradi huu wa mabilioni ya fedha na kuwachukulia hatua za kisheria.

Inawezekana hili nalo likapita tu…