Pastor Solly Mahlangu akionesha mbwembwe zake kwa mashabiki na wapenzi wa muziki wa injili kwenye Tamasha la Krismas jijini Dar es Salaam alipopanda jukwaani. Mwimbaji huyo toka Afrika Kusini alikuwa kivutio cha pekee kwenye tamasha hilo.
MWIMBAJI maarufu wa muziki wa injili kutoka nchini Afrika Kusini, Pastor Solly Mahlangu amekuwa kivutio kikubwa katika Tamasha la Krismas lililofanyika jijini Dar es Salaam. Pastor Solly Mahlangu alianza kushangiliwa na wananchi walioshiriki tamasha hilo mara tu baada ya MC kutangaza kuwa ilikuwa ni zamu yake kupanda kwenye jukwaa.
Idadi kubwa ya washiriki walisimama na kuanza kushangilia na kuimba naye kwa pamoja nyimbo zake alipoanza kutumbuiza jukaani. Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili anayeimba kwa kutumia lugha ya kiingereza aliwavuta zaidi washiriki baada ya kuanza kuimba kwa kiswahili baadhi ya nyimbo zake akizitafsiri.
Kitendo hicho kilileta mvuto zaidi na wananchi kuanza kuimba na kucheza nyimbo zake huku akiendelea kutoa burudani hiyo ya nyimbo za nchini. Waimbaji wengine waliovuta hisia za wanatamasha na kushangiliwa zaidi ni pamoja na Rose Muhando, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Edson Mwasabwite, John Lissu, Solomon Mukubwa (Kenya), Ephraim Sekeleti (Zambia) na Liliane Kabaganza (Rwanda).
Akizungumza katika tamasha hilo, mgeni rasmi Waziri wa Nchi, Sera Uratibu na Bunge, William Lukuvi aliishukuru kampuni ya Msama Promotions kwa kuandaa tamasha hilo linalowaleta pamoja Watanzania katika kusherehekea Siku Kuu ya Krismas pamoja na kusisitiza amani kupitia jumbe zake.
Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha sherehe zote za Siku Kuu za Mwisho wa Mwaka yaani Krismas na mwaka mpya zinasherehekewa kwa amani na utulivu kutokana na ulinzi iliouimarisha maeneo yote ya nchi. “…Sherekeeni kwa amani na utulivu bila woga wowote maana Serikali imeimarisha ulinzi wa kutosha kuanzia hapa tulipo hadi nyumbani kwenu,” alisema Lukuvi.
Tamasha la Krismas mwaka huu pia litaendelea kufanyika mikoa ya Morogoro tarehe 26, Tanga (28), Arusha (29) pamoja na Mkoa wa Dodoma tarehe Mosi ya Mwezi Januari. Naye Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuiunga mkono katika uandaaji wa matamasha hayo yanayofanyika kila mwaka kwenye siku kuu za Krismas na Pasaka.