*Kocha Simba awashangaa wachezaji wake
KOCHA wa Yanga, Kosta Papic ameomba radhi kwa matokeo mabaya iliyopata timu yake kwa mchezo wa kwanza wa raundi ya awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri.
Katika mchezo huo ambayo Yanga imejiweka njia panda, inahitaji ushindi ama sare ya 2-2 iweze kusonga mbele. Kwa kanuni za mashindano hayo, endapo mechi hiyo itasimama suluhu, basi Yanga itakuwa imeaga michuano hiyo kwa kuwa Zamalek itakuwa na faida ya bao la ugenini.
Yanga iliyokosa mabao matano ya wazi, ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 36 lililofungwa na Hamisi Kiiza baada ya kupiga mpira wa mbali uliodhaniwa unatoka na kujaa wavuni.
Hata hivyo, Amr Zaki aliyeingia kipindi cha pili, aliisawazishia bao timu hiyo ambayo marudiano yake yatakuwa baada ya wiki mbili.
Papic alisema: “Matokeo haya ni mabaya sana, naomba rad hi mashabiki, viongozi na wale wote wapenzi wa Yanga, lakini nitakachofanya ni kuitengeneza safu ya ushambuliaji.
“Tumetengeneza nafasi nyingi, lakini wachezaji wangu walikosa umakini na kushindwa kufunga…katika siku 10 za maandalizi ya mechi ya marudiano, naamini makosa yaliyojitokeza tutayarekebisha, nitakomalia washambuliaji,” alisema Papic.
Papic ambaye alionekana kuchanganywa na kelele za mashabiki wa Simba kuwashangilia wapinzani wake, alisema kuwa atahakikisha anawashughulikia wachezaji wake kwa kuwa kazi kubwa ni kuwatoa Zamalek.
Hata hivyo, alisema kuwa nafuu yake ni Zamalek kucheza bila mashabiki, lakini pamoja na hayo alisema kukosa nafasi za kufunga kwa wachezaji wake kumewaweka katika mazingira magumu ya mchezo wa marudiano.
Wakati huo huo mwandishi kutoka Kigali anaripoti kuwa KOCHA wa Simba, Cirkovic Milovan amewashangaa wachezaji wake kwa kushindwa kufuta maelekezo katika kipindi cha pili na kuruhusu Kiyovu kupata bao la kusawazisha kwa Kiyovu.
Akizungumza na Mwananchi, Milovan alisema sifahamu kiliwakuta kitu gani kwani walicheza kama wamechanganyikiwa hadi muda wote wa kipindi cha pili wakaamua kukaa nyuma tu.
“Sikuwaambia kwamba tunaingia kipindi hiki kwa lengo la kujilinda na wote tukae nyuma na kupiga mipira mirefu mbele kusipokuwa na mtu.”
Alisema niliwataka wacheze mpira wa chini na kufanya mashambulizi kama walivyooanza mpira, lakini wenyewe wote waligeuka na kukaa golini kwao, hata alipofanya mabadiliko bado waliongia walishindwa kuonyesha tofauti.
Katika mchezo huo Milovan alimtoa Ramadhani Singano, Shomari Kapombe na Felix Sunzu na kuwaingiza Johas Gerald, Uhuru Selemani na Victor Costa.
“Nadhani hapo ndipo tulipokosea na kutoa mwanya kwa wenzetu kutulia na kufanya mashambulizi mengi na hatimaye kupata goli la kusawazisha,” alisema Milovan
“Wapinzani wetu waligundua udhaifu wetu wao wakajiamini kuliko sisi, ila nashukuru kwa kupata pointi moja hapa tunajipanga na mechi ya marudiano.
Naye kiungo Kapombe alisema walicheza kwa kukosa umakini na kushindwa kujituma kama kawaida yao katika kipindi cha pili.
“Tulibweteka na bao tulilolipata na kudhani kwamba mechi imekwisha kumbe sivyo, pia hatukufuta maelekezo ya kocha ndio maana muda wote tulikuwa nyuma.
“Kwa upande mwingine nadhani hali ya hewa imechangia kwani kipindi cha pili tulikuwa tunaonekana kukosa kasi yetu ya kawaida kutokana na kubanwa na pumzi,” alisema Kapombe na kuungwa mkono na chipukizi mwenzake Singano.
“Hii baridi ya huku ilinipa wakati mgumu sana kwani kuna wakati nilijihisi kukosa pumzi na kupata tabu kupumua.”
Singano aliyeichezea Simba mechi yake ya kwanza ya kimataifa ya mashindano alimshukuru kocha wake Milovan kwa kumpa nafasi ya kucheza.
“Namshukuru kocha kwa kuniamini na kunipa muda wa kucheza hapa,, naamini akiendelea kunipa nafasi hivi nitacheza vizuri zaidi, japokuwa mabeki wa Kiyovu walikuwa wananishinda nguvu ila hayo yote ni mambo ya mazoezi nitakuwa fiti.”
Kwa matokeo hayo Simba sasa inahitaji kushinda au kutoka suluhu ili iweze kufuzu kwa hatua ya 16 bora ya michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika.
CHANZO: Mwananchi (www.mwananchi.co.tz)