MWANAMUZIKI nguli wa dansi kutoka nchini Congo DR, Papa Wemba ni miongoni mwa wasanii wanaotarajia kutumbuiza katika tamasha kubwa la Kimataifa la Muziki la ‘Karibu Music Festival’ linaloratibiwa na Karibu Cultural Promotions Organization (KCPO) na Legendary Music Entertainment and Promotions Co. Ltd.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Ofisa Mauzo wa KCPO, Ernest Biseko alisema wanamuziki wengine na bendi zinazotarajia kutumbuiza katika tamasha hilo ni pamoja na Sarabi Band, H-Art The Band, Yuzzo & Frontline Band. Alisema wasanii kutoka Tanzania watakaotumbuiza ni pamoja na Jhiko Manyika (Jhikoman) na band yake ya Afrikabisa, Tomgwa Ensembe, Misoji Nkwambi mshindi wa BSS 2008, Ze Spirit. Isha Mashauzi, Damian Soul na babd yake, Juma Nature, Msafiri Zawose na band yake.
Akifafanua zaidi Biseko alisema tamasha hilo la mwaka huu lenye kauli mbiu ‘Fahari ya Tanzania’ litafanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Novemba 6 hadi 8 mwaka huu katika viwanja vya Mwanakalenge karibu na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA).
“…Tamasha hili linalenga kukuza muziki wa Kiafrika na kuonesha tamaduni za Kiafrika kwa dunia nzima kupitia jukwaa la muziki litakalokutanisha wanamuziki kutoka sehemu mbalimbali duniani,” alisema Biseko.
Aidha alibainisha kuwa tamasha hilo ni sehemu ya kukutanisha wadau wote wa muziki kutoka dunia nzima, kubadilishana uzoefu wa kikazi na kufungua milango kwa wasanii kukuza mtandao wa marafiki na kujifunza vitu vipya toka wasanii wa je ya Nchi. Aliongeza kuwa wanamuziki wote watakaopanda jukwaani siku zote tatu za tamasha watatumbuzia na vyombo vyao ‘live’ na hakutakua na kutumia CD (playback).
Alisema tamasha litakua na nafasi za kibiahsara kwa wasanii kwani watapata fursa ya kuonesha kazi zao na kuuza album za miziki yao pamoja na wasanii wa kazi za mikono kuuza sanaa zao zitokanazo na bidhaa za asili kama vile uchongaji wa vinyago, michoro mbali mbali na urembo utokanao na vifuu vya nazi.
Miongoni mwa wadhamini wa tamasha waliopatikana hadi sasa ni pamoja na Jebel Coconut (SBL), Legendary Music, K.I. , Swiss Embassy, Precision Air, Greenpark Village Residence, Nafasi Art Space, Coca-Cola, Advertising Dar, Tanzanian Printers, Mwananchi Communications Limited, Kaya FM, Magic FM, Focus Outdoor, JOVAGO, Kaymu, na TiME Tickets.
Alisema mbali na tiketi kuuzwa katika vituo pia zinapatikana kwenye website ya http://karibumusic.org/.
Tamasha litaanza na matembezi kuashiria uzinduzi wa tamasha na litakuwa na mafunzo mbalimbali yenye mlengo wa kuwasaidia wadadu wa muziki kufahamu mambo anuai kwenye masuala ya kiutawala na jinsi ya kujitangaza, mambo ya hati miliki, ngoma za asili, kupiga ngoma, n.k.