Na Mwandishi Wetu
WAAMUZI kutoka Ethiopia ndiyo watakaochezesha mechi namba 7 ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Zamalek ya Misri itakayochezwa Februari 18 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na TFF, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Bamlack Tessema kuwa mwamuzi wa kati kwenye mechi hiyo wakati waamuzi wasaidizi ni Yilma Knife na Mussie Kindie.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura imesema, mwamuzi wa akiba (fourth official) atakuwa Waziri Sheha wa Tanzania na Kamishna wa mchezo huo ni Charles Kafatia wa Malawi.
Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa kozi ya ukocha ngazi pevu (advanced level) itakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Februari 12-25 mwaka huu.
Wakufunzi watakuwa Kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen ambaye pia ni mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni ambaye pia ni mkufunzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Kocha wa timu za Taifa za vijana Kim Poulsen ambaye pia ni mkufunzi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).
Mwisho wa kupokea maombi kwa makocha wanaotaka kushiriki kozi hiyo ambayo ada yake ni sh. 60,000 itakuwa Februari 5 mwaka huu. Sifa kwa waombaji ni kuwa elimu ya kuanzia kidato cha nne, wawe wanafanya kazi hiyo ya ukocha na wamefaulu vizuri mafunzo ya ukocha ngazi ya kati (intermediate level). Pia wawe wamefundisha angalau kwa miaka miwili baada ya kupata cheti cha intermediate level.
Pia wanatakiwa maombi yao yawe yameidhinishwa na ama vyama vya makocha wa mpira wa miguu vya mikoa, vyama vya mpira wa miguu vya wilaya au vyama vya mpira wa miguu vya mikoa. Kwa makocha watakaofaulu kozi hiyo watakuwa wamepata sifa ya kuhudhuria kocha ya ukocha ya Leseni C ya CAF.