Pambano la Cheka na Chimwemwe Kudumisha uhusiano kati ya TZ na Malawi

MPAMBANO wa kugombea ubingwa wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati utafanyika wakati kukiwa na mzozo wa mpaka wa ziwa Nyasa kati mya Tanzania na Malawi.
Mpambano huo unaowakutanisha Mtanzania Francis Cheka na Mmalawi Chimwemwe Chiotra unafanyika katika jiji la Arusha na linategemea kujenga uhusiano kati ya nchi hizi mbili zenye mahusiano ya muda mrefu.
Bondia Chimemwe Chiotra ni mwanajeshi kutoka katika jeshi la Malawi na alianza harakati zake katika ngumi za kulipwa mapema kabisa na kujizolea sifa kemkem ambazo zimemwezesha kukubaliwa na IBF kugombea mkanda wake.
Chimwemwe aliingia katika jiji la Arusha kwa mbembwe tarehe 20 akifuatana na kocha wake Daudi Kikwanje na kudai kuwa wamekuja kuuchukua mkanda huo wa IBF waupeleka nchini Malawi ambako ndipo unapostahili kukaa.
Naye Francis Cheka ambaye ni bingwa wa mikanda mingi pamoja na IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati ametamba kumwonyesha mwanajeshi huo wa jeshi la Malawi jinsi ngumi zinavyotakiwa kuchezwa. Cheka ametamba kuwa ataubakiza mkanda huo hapa Tanzania kwani ndipo mahala unapostahili kukaa!
Mpambano kati ya Francis Cheka na Chimwemwe Chiotra wa Malawi umekuwa gumzo kubwa katika jiji la Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma pamoja an chi jirani za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.
Wapenzi wengi kutoka maeneo hayo wanategemea kufurika kwa wingi jijini Arusha tayari kuushughudia mpambano huo uliopewa jina la “Vurumai chini ya Mlima Meru” na wakazi wengi wa jiji hilo lililofunguliwa rasmi kuwa jiji hivi karibuni.
Viongozi wengi wakiongozwa na Meya wa jiji la Arusha Gaudence Lyimo watahudhuria mpambano huo ambao utafungua rasmi jiji la Arusha kuwa Las Vegas ya ngumi katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati.
IBF imewateua Onesmo Ngowi kuwa msimamizi mkuu akisaidiwa na Nemes Kavishe(Refarii), Boiniface Wambura (Jaji), Mark Hatia (Jaji) na Galous Lingongo kutoka jiji la Tanga kama jaji.
Nayo TPBC imewateua pia waaamuzi hao kusimamia mapambano ya utangulkizi.