Pakistan kuifungua tena njia ya misafara ya NATO

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Pakstan

WAZIRI wa Mambo ya Nchi za Nje wa Pakistan amesema wakati umewadia kufungua njia ya misafara ya NATO kuelekea Afghanistan, akisema Serikali imetoa ujumbe unaoeleweka kwa kuifunga njia hiyo, ikilipiza kisasi kwa mashambulizi ya Marekani yaliyouwa wanajeshi wa Pakistan.

Kauli ya waziri huyo, Hina Rabbani Khar, inaonesha kuwa shinikizo la Marekani dhidi ya Pakistan limefanikiwa, ingawa hadi sasa Marekani imakataa kuomba radhi kwa mashambulio hayo yaliyofanywa na ndege zisizo na rubani, kama ilivyotakiwa na bunge la Pakistan.

Hatua ya kuifungua tena njia hiyo itapokewa vibaya nchini Pakistan ambako bado kuna hisia kali dhidi ya Marekani, na watu wenye msimamo wa kiislamu bado wanakasirishwa na mashambulizi hayo ya Marekani yaliyouwa wanajeshi 24 wa Pakistan mwezi Novemba mwaka jana. Marekani imesema mashambulizi hayo yalifanywa kwa bahati mbaya.
-DW