Paka Amponza Mfugaji, Amfunga Miaka 3 Jela

Paka

Paka

MAHAKAMA ya mwanzo Mengwe wilayani Rombo imemhukumu mkazi wa Rombo, Godfrey Kimaryo(32) kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya shambulio la mwili kwa kumjeruhi vibaya mtoto wa miaka tisa kwa madai kua aliiba paka wake.

Hukumu hiyo imetolewa na hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mengwe, Adinani Kingazi kesi ambayo ilivuta hisia za watu wengi wa Wilaya ya Rombo ambao walifurika mahakamni hapo kusikiliza hukumu hiyo.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mnamo Septemba 29, 2014 majira ya saa kumi na mbili unusu jioni huko katika Kijiji cha Mamsera Juu, mshatakiwa alifanya kosa hilo kinyume na kifungu 241 cha sheria ya makosa ya jinai sura ya 16 kanuni ya adhabu.

Imedaiwa mshtakiwa bila halali na akijua kufanya hivyo ni kosa alimshambulia kwa mateke na ngumi pamoja na kumng’ata kwa meno mgongoni, Dilex Lyakurwa (09) hali ambayo ilimsababishia maumivu makali.

Kingazi alisema mshtakiwa alimshambulia mtoto huyo kwa kile alichodai kuwa alienda kuchota maji nyumbani kwa mshtakiwa na wakati alipokua akirudi paka wa mshtakiwa alimfuata mtoto huyo hivyo alipomrudisha paka huyo aligoma ndipo mshtakiwa alikasirika na kumshambulia kwa madai kua amemwibia paka wake.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu, Adinani Kingazi alisema mahakama hiyo imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka pamoja na kielelezo cha fomu no PF3 iliyotolewa na daktari ambayo inaonesha mtoto huyo aliumizwa katika bega la kushoto na mkono wa kushoto. Pia ilionesha alichomwa na kitu chenye ncha kali mgongoni.

Alisema kuwa kitendo hicho ni cha kinyanyasaji na kinakiuka sheria ya watoto ya mwaka 2009 na pia alieleza mahakama hiyo imeshangazwa na kitendo kilichofanywa na mshtakiwa cha kumtesa mtoto kwa sababu ya paka na kusema kuwa jambo hilo haliingii akilini kwa mtu mwenye akili timamu.

Aliongeza kuwa mshtakiwa atatumikia jela miaka mitatu na baada ya kumaliza adhabu hiyo atamlipa mlalamikaji kiasi cha shilingi laki mbili kama gharama za matibabu na fidia na maumivu aliyoyapata kwa kitendo hicho cha kinyama. Hata hivyo alisema adhabu hiyo itathibitishwa na Mahakama ya wilaya kwa ajili ya utekelezaji kwa kuwa mahakama hiyo ya mwanzo haina mamlaka ya kudhibitisha adhabu kubwa.