KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa mapendekezo ya kuinusuru Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kutokana na hali mbaya ya kampuni hiyo kifedha kwa sasa ambapo inaendeshwa kwa hasara huku ikiwa na madeni makubwa. PAC imetoa mapendekezo hayo katika taarifa yao kwa bunge ya mwaka juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mashirika ya umma iliyotolewa Januari 28 mwaka 2015.
Kwa mujibu wa taarifa ya PAC hali ya mapato na matumizi ya TTCL kwa mwaka 2012 ilipata hasara ya bilioni 20.883 huku kwa mwaka 2013 ikipata hasara ya bilioni 16.258. PAC ilisema majumuisho ya hasara ya TTCL kupata hasara kwa takribani kwa miaka 10, Kampuni sasa imekuwa na hasara ambayo kwa mwaka 2013 ilifikia bilioni 334.48, jambo ambalo limeiondolea mvuto wa kukopeshwa na taasisi za fedha hata zile zenye nia ya kuikopesha.
“…Ukosefu wa fedha za kutosha kutekeleza miradi ya Kampuni umekuwa kikwazo kwa TTCL kukabiliana na ushindani wa kibiashara. Kwa kipindi kirefu ufanisi wa TTCL kiuwekezaji na kifedha umeendelea kudorora. Tangu TTCL ibinafsishwe mwaka 2001, hakuna uwekezaji mkubwa uliofanyika na mpango wa kutafuta mkopo kutoka mabenki ya ndani na nje ya nchi unakwamishwa na masharti ya kupata udhamini wa Serikali,” ilieleza taarifa hiyo ya PAC.
PAC iliongeza kuwa ukiacha madeni yaliopo pia TTCL inadaiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) jumla ya bilioni 25 hivyo kufanya jumla ya deni kufikia bilioni 101.6. Kamati hiyo ya bunge imesema kuna umuhimu wa Serikali kufanya maamuzi ya haraka ya kuikwamua TTCL ili iweze kuendelea kutoa huduma kwenye Sekta ya Mawasiliano ikizingatiwa kuwa ndiyo inayoendesha Mkongo wa Taifa wa mawasiliano.
Katika mapendekezo ya PAC ili kuikwamua TTCL imeishauri Serikali kununua hisa asilimia 35 zinazomilikiwa na Bharti Airtel katika TTCL kwa gharama ndogo kwani Bharti Airtel haikutimiza kikamilifu masharti ya mkataba wa mauziano ya hisa hizo hapo awali kwani tangu inunue hisa hizo haijafanya uwekezaji katika Kampuni ya TTCL.
“…TTCL isamehewe deni la Serikali Sh. 76.6 bilioni na deni la TCRA Sh. 25 bilioni ambayo jumla yake ni Sh. 101.6 bilioni na fedha hizo zipelekwe kuongeza mtaji ili Kampuni itoke kwenye kuwa na mtaji hasi wa Sh. 87.896 bilioni na kuwa na mtaji chanya wa sh. 13.704 bilioni. Likifanyika hili basi Kampuni hiyo itaweza kukopesheka. Serikali ikamilishe taratibu zake za kuimilikisha TTCL Mkongo wa Taifa ili izidi kuuendeleza kwa ufanisi na kuongeza mapato ya TTCL,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo PAC imeshauri kuwa kuna umuhimu wa kufanya marekebisho ya muundo wa Kampuni ya TTCL kwani kwa sasa ina idadi kubwa ya wafanyakazi (1549) isiyoweza kuwalipa. Aidha, ilibainisha kuwa kwa sasa zinahitajika bilioni 32 kwa ajili ya kugharamia urekebishaji wa muundo wa Kampuni ili uendane na mahitaji ya utoaji wa huduma mbalimbali.
Mashirika mengine yenye hali mbaya kifedha na uendeshaji ni pamoja na Shirika la Ndege Tanzania, ATCL ambayo kwa sasa ina madeni makubwa huku ikiwa na ndege moja aina ya Dash 8–Q 300, Wafanyakazi 142 na Jengo la ATC House lililoko mtaa wa Ohio, Dar es Salaam.