VIONGOZI wa mataifa 11 ya eneo la Maziwa Makuu wanatarajiwa kukutana mjini Kampala Uganda kwa kikao cha dharura kutafuta suluhu la mzozo wa kivita unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Rwanda inashutumiwa kuwasadia waasi wa kundi la M 23 wanaopigana na vikosi vya Serikali, shutuma ambazo inapinga vikali.
Wakati huo huo shirika la Oxfam linasema mamilioni ya watu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wako chini ya udhibiti wa makundi ya wanamgambo yanayowaingiza kwa nguvu watoto vitani, kufanya uporaji na ubakaji.
Shirika hilo la misaada linasema mateso dhidi ya binadamu yanaendelea kushamiri mashariki mwa congo. Shirika la Oxfam linasema kuwa serikali ya jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imepoteza uthibiti katika maeneo mengi ya mashariki mwa taifa hilo na hali ya usalama ni ya kutamausha.
Shirika hilo linasema eneo hilo limetumbukia katika vurugu. Watu wanauwawa, wanawake wanabakwa huku mali zikiporwa. Wananchi wanaitishwa pesa kwa lazima. Haya yote yanafanyika bila kukemewa, shirika la Oxfam linasema.
Shirika hilo la kutoa msaada limeeleza kuwa hali hiyo imesababishwa na harakati za sasa za kukabiliana na kundi la waasi la M23 lililoanzisha uasi wake mashariki mwa Congo mwezi Aprili Mwaka huu.
Hii imepelekea vikosi vya usalama kujiondoa katika maeneo mengine yenye mzozo mashariki na kuyaachia makundi ya wanamgambo kupagania uthibiti wa vijiji pamoja na miji katika eneo hilo.
Shirika la Oxfam linasema takriban watu milioni moja wamekimbia makaazi yao katika kipindi cha miezi minne iliyopita, na hali ya kibinadamu ni mbaya. Maradhi ya kipindupindu yanatishia kuangamiza maelfu ya watu na hali mbaya ya kiusalama imefanya vigumu msaada kutolewa kwa watu wanao-uhitaji.
Shirika la Oxfam sasa linatowa wito wa swala la kulinda raia kupewa kipaumbele kwenye ajenda ya kongamano la mataifa ya maziwa makuu linaloanza hivi leo mjini Kampala Uganda.
-BBC