MWANARIADHA mlemavu wa Afrika Kusini Oscar Pistorious atauza nyumba yake ili aweze kumudu gharama za kesi ya mauaji inayomkabili. Taarifa hii ni kwa mujibu wa wakili wake Brian Webber ambaye amenukuliwa na Shirika moja la habari SAPA akisema kesi hiyo itaendelea kwa zaidi ya wiki tatu zilizotarajiwa kwa kesi hiyo kukamilika.
Oscar hajaweza kurejea katika nyumba yake hata baada ya maofisa wa usalama kumruhusu arejee huko zaidi ya mwaka mmoja uliopita huku uamuzi ukitolewa wa nyumba ile kusalia ikiwa imefungwa hadi pale kesi hiyo itakapo kamilika.
Kwa Mujibu wa SAPA, hati za kortini zilizoandikishwa mwaka jana wakati mwanariadha huyo alipokuwa akiwasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana zaonesha kuwa nyumba hiyo iliyo katika Mtaa wa Silverwoods ina thamani ya Randi millioni 5 ambazo ni sawa na dola za Marekani 457, 000.
Oscar anakanusha madai ya kumuua mpenzi wake mnamo Februari 14, 2013 huku akisema kuwa alimpiga risasi kimakosa. Kesi ya mauaji dhidi yake ambayo kwa sasa iko katika wiki ya tatu, imehairishwa Jumatatu ambapo mashahidi wengine watano wa upande wa mashitaka wanatarajiwa kutoa ushahidi wao kabla ya yeye kupewa fursa ya kujitetea.
Upande wa mashitaka unadai kuwa Pistorious alimpiga risasi Bi. Reeva Steenkamp, aliyekuwa mwana mitindo, mtangazaji maarufu wa runinga na mwana sheria baada ya kinachodhaniwa kuwa ugomvi wa kimapenzi nyumbani.
Huku kwa upande wake, Pistorious anasema kuwa aliamini kuwa mpenzi wake alikuwa amelala na akidhani kuwa palikuwa na mwizi nyumbani kwake alifyatua risasi kuelekea chooni asubuhi mapema mnamo Februari 14, 2013. Iwapo mwanariadha huyu mwenye umri wa miaka 27 atapatikana na hatia, huenda akakabiliwa na kifungo cha maisha.
-BBC