MWANARIADHA nyota wa nchi ya Afrika Kusini Oscar Pistorius amehukumiwa kwenda jela miaka 5 baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mpenziwe Reeva Steenkamp bila kukusudia. Hukumu hiyo imetolewa baada ya mwanariadha huyo mlemavu kuthibitika kuwa alifanya mauaji hayo bila ya kukusudia.
Jaji Thokozile Masipa akitoa hukumu hiyo alianza kwa kueleza kuwa itakuwa ni vigumu na changamoto kwake kutoa hukumu ambayo itaweza kuridhisha pande zote za kesi. Upande wa mashitaka ulitaka mwanariadha huyo kupewa kifungo cha miaka 10 gerezani baada ya kupatikana na makosa ya kuua bila kukusudia.
Hata hivyo katika utetezi wake Pistorius alisema kuwa alifyatua risasi baada ya kudhani kuwa jambazi alikuwa amevamia nyumba yake. Upande wa mashitaka ulisisitiza Pistorius afungwe jela wakati wakili wa Pistorius wakimtaka jaji ampe kifungo cha nyumbani cha miaka mitatu na pia apewe usaidizi na ushauri wa kubadili tabia yake.
Jaji alisema kuwa Pistorius asingepewa adhabu ya kifungo cha nyumbani kwani hukumu kama hiyo ingekuwa hatua mbaya na mfano mbaya kwa wahalifu jambo ambalo hakuliridhia hata kidogo katika kesi hiyo.
-BBC