KAMPUNI ya Oracle Sytem Limited kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano itakuwa na mkutano wa The Africa Security Summit utakaofanyika hoteli ya Kilimanjaro, Dar es Salaam tarehe 30 Juni, 2016. Lengo la mkutano huu ni kuwakutanisha wadau na wataalamu mbalimbli wa Taasisi za Serikali na sekta binafsi wapatao watu 200 kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Oracle system Ltd wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, Afrika, Cherian Varghese, akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano, Prof. Faustin Kamuzora lengo la mkutano huo ni kushirikiana na Serikali ya Tanzania na kuendeleza Sekta ya Mawasiliano.
Varghese alisema kuwa mkutano huo utawawezesha wataalamu wa watanzania na kuwajengea uwezo na kuongeza uelewa wa usalama wa taarifa na umuhimu wake na namna ya kuzitumia ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya Taifa letu. Pia Kampuni yake imetambua na kuona namna ambavyo Tanzania imewekeza na kuthamini Sekta ya Mawasilino kwa kuwa na miundombinu ya kisasa, Sera, sheria na kanuni zinazosimamia Sekta ya Mawasiliano na kutambua mchango wake katika kukuza uchumi.
Prof. Kamuzora aliwaahidi kuwa Wizara itawapatia ushirikiano wa kutosha ili Taifa liweze kunufaika kupitia utaalamu, ujuzi na weledi wa Kampuni ya Oracle ili kuendeleza Sekta ya Mawasiliano nchini. Kampuni hiyo tayari imewekeza na kushirikiana na nchi nyingine za Afrika ikiwemo Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Kenya na Uganda kuendeleza Sekta ya Mawasiliano katika maeneoe ya usalama wa taarifa na kuongeza ukusanyaji wa mapato kutumia njia ya kielektroniki.