SEKTA ya Usafirishaji nchini inakabiliwa na changamoto kubwa na ipo katika tishio la kuanguka kutokana na kuongezwa kwa kodi mbali mbali zitokanazo na bajeti ya mwaka huu na hivyo kufanya wamililiki wa magari ya usafirishaji kupitia katika wakati mgumu sana kibiashara hasa kwa kuzingatia ushindani uliopo katika biashara hiyo Afrika mashariki.
Kilio hicho cha wasifirishaji hao kiliwasilishwa jana mbele ya kamati maalum ya bajeti ya bunge na viongozi wa juu wa chama cha wamiliki wa magari ya usafirishaji nchini Tanzania Truck Owners Association (TATOA) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Seif. A. Seif. Katika mkutano huo, TATOA ilieleza changamoto yake juu ya mustakbali wa sekta ya usafirishaji na hofu ya kuanguka kwa sekta hiyo kufuatia ongezeko la kodi na tozo nyingi na hivyo kupelekea kuanguka kwa uchumi wa Taifa.
TATOA waliweka wazi kwamba kwa muda mrefu wamefanya juhudi na kazi kubwa sana ya kushinda changamoto nyingi zilizokuwa zinaiathiri sekta hiyo kwa muda mrefu kwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine. Mpaka kufikia sasa Juhudi hizo zimeweza kuzaa matunda na kuifanya sekta hiyo kuwa ni sekta ya pili nchini katika kuchangia pato la taifa ukilinganisha na ukweli kwamba ilikuwa ni sekta ya tano miaka michache iliyopita. Hivyo basi TATOA inaona kwamba hatua ya serikali kuongeza kodi hizo kwa mpigo bila ya kuzingatia changamoto zilizoko kunatishia kuirudisha nyuma sekta hiyo na hata kuathiri uchumi wa taifa kwa kiwango kikubwa.
Ukweli unabakia kwamba maendeleo ya kiuchumi ya taifa letu yanategemea kwa kiwango kikubwa ukuaji na ufanisi katika sekta ya usafirishaji hasa ukizingatia kwamba ufanisi wa sekta zote zingine kiuchumi unategemea kwa kiwango kikubwa ufanisi wa sekta ya usafirishaji. Hii inamaanisha kwamba, athari zozote katika sekta ya usafirishaji itagusa sekta zingine zote kiuchumi.
Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hii kwa uchumi wa taifa, TATOA kwa kushirikina na serikali ilichukua hatua za msingi ambazo lengo lake ni kuleta mabadiliko makubwa kwa wasafirishaji. Moja ya hatua hizo ni kutembelea nchi zote za jirani na Tanzania kwa lengo la kuinadi bandari yetu ya Dar es Salaam ili kuvutia nchi hizo kuitumia kupitishia mizigo yao kwa wingi ili kuongeza pato la taifa.
Ikumbukwe kuwa sekta ya usafirishaji inatoa ajira ya vijana Zaidi ya milioni moja nchini. Hatimaye, juhudi hizo zimeweza kuzaa matunda ya kutosha ambapo sasa utendaji na ufanisi wa bandari ya Dar es salaam umeongezeka kwa kiwango kikubwa sana na nchi kwa ujumla imeweza kufaidika na matunda hayo kimapato. Hata hivyo, katika hali iliyopo hivi sasa ambapo gharama za uendeshaji katika sekta hii zinaongezeka haraka hasa kupitia kuongezwa kwa kodi mbali mbali, kunaweza kuifanya Tanzania kurudi nyuma kiuchumi kwa haraka sana na kufanya juhudi zote zilizochukuliwa mpaka sasa kupotea bila faida.
Viongozi wa TATOA walitoa tahadhari kwa serikali kwamba ongezeko la kodi mbali mbali lililofanywa mwaka huu halikuzingatia ukweli kwamba tayari kuna utitiri mwingine mkubwa wa kodi nyingi ambazo kwanza tayari zilikuwepo toka mwanzo na pili nyingi ya hizo pia zimeongezwa kwa kiwango kikubwa. Baadhi ya kodi hizo ni kama ifuatavyo:
1. Kuongezeka kwa muundo wa kodi ya mafuta katika bajeti ya 2013/14
2. Kuongezeka kwa gharama za bima
3. Kuongezeka kwa kiwango cha Vehicle Road License katika bajeti ya 2013/14
4. Kuongezeka kwa mishahara ya wafanyakazi
5. Kuongezeka kwa gharama za tairi za magari na vipuri vyake
6. Kuongezeka kwa gharama za Sumatra
7. Kurudishwa kwa withholding tax
8. Kuongezeka kwa gharama za benki na riba kwa mikopo
9. Kodi zote za kawaida katika biashara
TATOA kwa kuzingatia hali halisi iliyopo na kwa kuzingatia athari mbaya za kiuchumi zitakazotokea endapo hatua muafaka hazitachukuliwa katika jambo hili, imewasilisha maombi yake mbele ya kamati maalum ya bajeti ya bunge la Tanzania ili iweze kuchukua hatua muafaka kuokoa mustakbali wa sekta hii kwa uchumi wa taifa.