*Abuni njia mpya kudhibiti ajali
Na Joachim Mushi
ONGEZEKO la ajali za barabarani zimemkera Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha na sasa amependekeza utaratibu mpya ambao unaweza kudhibiti matukio mengi ya ajali hizo.
Waziri Nahodha ambaye ndiye mwenye mamlaka ya usimamizi wa sheria barabarani kupitia Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, amepende sasa kuanza utaratibu wa magari na madereva hasa wa vyombo vya abiria kukaguliwa kila wanapoingia mkoa mmoja na kutoka.
Waziri Nahodha amesema hayo leo alipokuwa akizindua kampeni za Unywaji wa Pombe Kistarabu Zilizoanzishwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti nchini (SBL), zikiwa na malengo ya kupambana na matukio ya ajali za kizembe zinazofanywa na baadhi ya raia.
Akifafanua zaidi katika utaratibu huo, Nahodha amesema magari yote yawe ya mizigo na abiria yatakuwa yakikaguliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) husika pamoja na Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa (RTO) kabla ya kuendelea na safari kila linapoingia na kutoka ndani ya mkoa wao.
Amesema katika utaratibu huo polisi wanaweza kuwa wakipata taarifa za mwenendo wa magari barabarani kutoka kwa abiria ama kubaini wenyewe hali itakayosaidia kupunguza matukio ya ajali nchini.
“Mimi siridhishwi kabisa na visingizio vinavyotolewa na baadhi ya askari, eti kwamba wanashindwa kutambua mwendo kasi wa gari na hata ulevi wa dereva kwa kukosa vifaa…hii haiingii akilini kwangu. Naamini mtu mlevi au gari linalokwenda mwendo kasi unaweza kubaini haya kwa akili ya kawaida tu, haiitaji vifaa…hata mtoto mdogo anaweza kubaini huyu ni mlevi,” alisema Nahodha.
Amesema mkoa ambao utaendelea kuwa na matukio mengi ya ajali baada ya muda itaashiria kuwa Kamanda wa mkoa huo, RPC na RTO wameshindwa kazi hivyo hawana budi kuwapisha wengine ili waweze kufanya kazi kiufasaha. “Haiwezekani gari zipite mikoa hiyo bila kukaguliwa alafu zije kuleta ajali na kupoteza maisha ya watu na mali zao…, visingizio kwamba hatuna vifaa viishe mara moja kwani kumtambua mlevi hauitaji kifaa maalumu,” alisema waziri huyo.
Alisema lengo la Wizara yake ni kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, 2011 wanapunguza matukio ya ajali kwa asilimia 50. Amesema Polisi watafuatilia taarifa za madereva wa magari na watakapo jiridhisha wanafanya makosa hovyo watazifungia leseni zao bila ushahidi wa mahakama moja kwa moja.
“Tupeni taarifa za watu wanaofanya vibaya tutawafungia, bora lawama kuliko tuendelee kupoteza ndugu zetu kwa matukio ya ajali,” alisema. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa 2006 nchini kati ya matukio ya ajali 17,677, asilimia 78 ya matukio hayo yalichangia na sababu za kibinadamu ukiwemo ulevi. Aliipongeza SBL kwa uamuzi wake wa kufanya kampeni za kupinga unywaji wa pombe usio wa kistarabu kwani unachangia matukio ya ajali.
Katika kampeni hizo, SBL inasema rafiki mzuri hawezi kumuacha rafiki yake aendeshe gari huku akiwa mlevi, kwani atakuwa anahatarisha maisha yake na wengine kwa namna moja ama nyingine. Elimu itakayotolewa katika kampeni hizo itasaidia kupunguza matukio ya ajali yanayoweza kuzuilika, jambo ambalo litalinufaisha Taifa.