Ole Sendeka asema CCM isisubiri kuwajibiswa na wananchi

Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher ole Sendeka

Na Joachim Mushi

MBUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Simanjiro, Christopher ole Sendeka amesema CCM isingoje kuwajibishwa na Wananchi bali ihakikishe inawang’oa mafisadi wote ndani ya chaa hicho ili kurudisha imani kwa wananchi na wanachama wake. Hata hivyo amesisitiza kuwa suala la kujivua gamba lisiishie ndani ya chama bali hadi serikalini.

Sendeka ametoa kauli hiyo leo mjini hapa alipokuwa akizungumza na wanahabari mara baada ya kumalizika kwa mjadala wa maadhimisho ya miaka 12 ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julias Kambarage Nyerere uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambao ulishirikisha wanaharakati, wasomi anuai, wananchi na wanafunzi kutoka shule za sekondari jijini Dar es Salaam.

Amesema Nyerere alikiacha chama kikiwa na maadili ya hali ya juu na enzi zake alikuwa na msimamo juu ya kuwajibishana inapotokea kiongozi yeyote ameenda kinyume na maadili. Alisema hali hiyo ilionekana wazi kwani wapo baadhi ya viongozi waliwajibishwa enzi hizo hivyo chama kujenga imani kubwa kwa wanachama wake.

Kada wa CCM (kulia), Kingunge Ngombale Mwiru akiwa na Mweyekiti wa Taaluma ya Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Prof. Issa Shivji katika mjadala wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 12 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.


Amesema chama kimepita katika msukosuko mkubwa kufuatia dhana ya kujivua gamba, lakini utaratibu huo usiishie ndani ya chama pekee bali hata kwa viongozi na watendaji wa Serikali ya CCM- ambapo wamekuwa wakiboronga na kuitia hasara Serikali.

“Mimi huwa napenda kumnukuu Mwl. Nyerere; katika uhai wake aliwahi kusema kwamba chama madhubuti huzazaa Serikali madhubuti na vivyo hivyo chama regerege huzaa Serikali regerege…sasa chama lazima kiisimamie Serikali kuhakikisha inafanya yale yanayokubaliwa na chama,” alisema Sendeka.

Amesema chama kimewekwa madarakani na wananchi hivyo kutokana na kukithiri kwa hali ya ukiukaji maadili kwa viongozi kisingoje kuwajibishwa na wananchi bali kiwaengue wasiofaa, ili kujenga imani kwa wapiga kura.
Naye Kada Maarufu wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru ambaye ni miongoni mwa viongozi waliotoa mada katika mjadala huo alisema kuna kila sababu ya kuanza kuazimisha kumbukumbu za kifo cha Mwl. Nyerere kwa kudumisha maadili, kwa lengo la kumuenzi zaidi.

Wananchi mbalimbali wakiwa katika mjadala wa Mwalimu Julius Nyerere ulioandaliwa kuazimisha miaka 12 ya kifo chake.


Miongoni mwa washiriki wa mjadala huo pia alikuwepo Profesa Issa Shivji, madaktari na maprofesha kutoka chuo cha UDSM, viongozi mbalimbali wa vyama, wanaharakati na wanafunzi anuai.