Ole Naiko Apewa Tuzo ya Utumishi Bora Serikalini

ABG’s Director of Government Relations, Mr Emmanuel Ole Naiko (left), chats with the Permanent Secretary in the Prime Minister’s Office, Mr. Peniel Lymo (right), and other officials at a ceremony in Dar es Salaam recently to present Mr Ole Naiko with the 2012 Lifetime Achievement Award for Outstanding Public Service.

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mtendaji mstaafu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Emmanuel Ole Naiko, amechaguliwa kuwa mshindi wa kwanza wa tuzo ya utumishi bora wa umma kutokana na juhudi zake kubwa za kusaidia kukua kwa sekta binafsi nchini.

Tuzo hiyo ilitolewa kwa Ole Naiko na Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni binafsi nchini (CEO Roundtable of Tanzania) katika sherehe iliyofanyika Dar es Salaam Novemba 26 mwaka huu.

Akitoa tuzo hiyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Tanzania, Ali Mufuruki, alisema kuwa Ole Naiko amepewa heshima hiyo kutokana na rekodi yake mahiri alipokuwa serikalini kama mtetezi mkubwa wa sekta ya binafsi ili ishike nafasi yake kama injini ya ukuaji wa uchumi nchini.

“Kutokana na jitihada zako kubwa, serikali iliweka sera na kanuni nyingi ambazo zilisaidia kuvutia uwekezaji nchini Tanzania kutoka kwa kampuni za nje na za ndani,” alisema Mufuruki wakati akimwaga sifa kwa Ole Naiko.

Kwa upande wake, Ole Naiko aliushukuru Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni binafsi nchini kwa kutambua mchango wake na kumtunuku tuzo hiyo maalumu iliyotolewa kwa mara ya kwanza mwaka huu.

“Kuhusu hii tuzo yenye thamani kubwa kwangu ambayo mmenipa, napenda kusema kuwa nitakuwa daima nashukuru fursa nyingi ambazo nimepewa kulitumikia taifa langu. Hizi fursa nilizopewa zimekuwa ni za kipekee na zenye changamoto nyingi,” alisema.

Ole Naiko alisema kuwa akiwa mhandisi mwenye umri mdogo kwenye miaka ya 1980, alipata heshima kubwa ya kuteuliwa kuwa meneja mkuu wa mgodi wa dhahabu wa Buckreaf uliopo wilaya ya Geita ambao ulikuwa unamilikiwa na serikali.

“Nilisimamia shughuli za mgodi huu tangu ulipoanza mpaka tukaweza kuzalisha dhahabu mfululizo na kuipatia nchi yetu fedha nyingi za kigeni. Mpaka nilipoondoka kwenye mgodi wa Buckreaf mwaka 1989, bado mgodi ulikuwa unazalisha dhahabu,” alisema.

Baada ya kuongoza mgodi huo wa serikali, Ole Naiko alijiunga na Taasisi ya Kukuza Uwekezaji (Investment Promotion Centre) kilipoanzishwa na serikali mwaka 1990, kabla ya kugeuzwa kuwa Kituo cha Uwekezaji (Tanzania Investment Centre).

Akiwa TIC, Ole Naiko alifanya kazi miaka mingi kama Mkurugenzi wa Kukuza Uwekezaji na baadaye kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo.

Ole Naiko, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Mahusiano ya Serikali kwenye kampuni binafsi ya African Barrick Gold (ABG) baada ya kustaafu serikalini alitupilia mbali dhana kuwa viongozi wa zamani wa serikali walisaini mikataba mibovu kwenye sekta za madini na gesi.

“Watu wenye fikra hizo potofu wamesahau kuwa kabla ya mwaka 1998, hatukuwa hata na mgodi mmoja nchini uliokuwa unazalisha dhahabu. Ni baada ya kipindi hiki ndion Tanzania ikasonga mbele na kuwa moja ya nchi zinazoongoza Afrika kwa uzalishaji wa dhahabu,” alisema.

Alitoa changamoto kwa sekta binaafsi nchini kushirikiana na serikali kukuza ukuaji wa sekta ya kati kwenye uchumi wa Tanzania.

“Nawaomba mfanye kila linalowezekana kuisaidia serikali kwenye jitihada zake za kuendeleza kada ya kati nchini Tanzania,” alisema.