Ole Millya, Chatanda ‘wazichapa’ mkutano wavunjika

Na Mwandishi wa Thehabari, Arusha

TAARIFA zilizotufikia jana zinasema Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James ole Millya wanadaiwa kuzipiga ndani ya kikao cha NEC Mkoa kilichofanyika kwenye ukumbi wa CCM mkoani Arusha.

Chanzo cha habari cha dev.kisakuzi.com kilisema inadaiwa, Katibu wa Mkoa, Mary Chatanda ndiye alieanza kumrushia kibao Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa Ole Millya, ndipo naye akajibu mapigo kabla ya kikao kuvunjika.

Mvutano huo wa kupingana na viongozi kati ya UVCCM na CCM Mkoa huo umekuwa ukiibuka kila mara huku yakifanyika maandamano, ambapo hivi karibuni kundi la vijana wanane kutoka UVCCM mkoani hapa lilimlipua Katibu Chatanda mbele ya Tume ya Maadili na Usalama ya chama hicho kwa kudai kuwa katibu huyo ni mzigo.

Vijana hao walitoa madai hayo mbele ya tume hiyo na kutishia kwamba wako tayari kuhamia upinzani ikibidi endapo CCM kitaendelea kumkumbatia katibu huyo.Hatua hiyo imekuja mara baada ya tume hiyo kuweka kambi mkoani hapa kwa wiki moja sasa ikitokea Dar es Salaam.

Lengo la kamati hiyo ni kuyahoji makundi mbalimbali yanayosigana juu ya mvutano baina ya UVCCM na Chatanda. Kamati hiyo ilimaliza kuwahoji wahusika usiku wa manane kuamkia jana katika Ofisi za CCM Mkoa wa Arusha. Vijana hao wanane waliohojiwa, wanatuhumiwa kuendesha maandamano haramu Mei 19, mwaka huu.

Na Mwenyekiti wa UVCCM, Ole Milya alithibitisha taarifa za kubanwa kwa Chatanda na vijana hao wanane. Alisema msimamo wao wa kumtaka Chatanda aondoke madarakani uko palepale akidai kuwa amesababisha makundi miongoni mwa vijana na kuwachonganisha na viongozi wa dini na kusababisha Jimbo la Arusha Mjini kuchukuliwa na upinzani.

Hata hivyo juhudi za Thehabari kuwatafuta viongozi hao kuzungumzia tukio hilo jana hazikuzaa matunda baada ya kupiga simu zao zote za kiganjani ambazo hazikuwa zikipatikana, mtandao huu unaendelea kuwatafuta na utawajuza zaidi kitakachozungumzwa na viongozi hao.