Na Beatrice Lyimo, MAELEZO -DAR ES SALAAM
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa taarifa kuhusu mfumuko wa bei wa Taifa ambapo mfumuko wa bei wa taifa kwa mwezi oktoba, 2016 umebaki kuwa asilimia 4.5 kama ilivyokuwa mwezi Septemba mwaka huu Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mtakwimu Mkuu wa Ofisi ya Taifa takwimu, Ruth Minja alisema kuwa lengo la taarifa hiyo ni kuwafahamisha wananchi juu ya mfumuko huo wa bei pamoja na mwenendo wa mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki.
Aidha, alisema kuwa fahirisi za bei zimeongezeka hadi kufikia 103.17 mwezi oktoba,2016 kutoka fahirisi 98.72 mwezi oktoba 2015 ambapo mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi huo umebaki kuwa asilimia 6.0 kama ilivyokuwa mwezi Septemba mwaka huu. Katika hatua hiyo, Bi. Minja alisema kuwa mfumuko wa bei wa mwezi Octoba umechangiwa na kuongezeka kwa kasi ya bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi oktoba mwaka huu zikilinganishwa na bei za nmwezi oktoba 2015.
“Mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula zilionesha kuongezeka ni pamoja na bei za mahindi kwa asilimia 18.3, unga wa ngano kwa asilimia 4.8, samaki wabichi kwa asilimia 5.07” alisema Bi. Minja”
Alisema bidhaa nyingine ni ndizi ziliongezeka kwa asilimia 5.2 ambapo kwa bidhaa zisizo za vyakula zilionesha kuongezeka ni pamoja na bei za mkaa kwa asilimia 15.4 na vyakula kwenye migahawa kwa asilimia 17.3. Akizungumza kuhusu mabadiliko ya bei kati ya mwezi septemba na octoba mwaka huu, Bi Minja alisema kuwa fahirisi za bei zimeongezeka hadi 103.17 mwezi octoba 2016 kutoka 103.05 mwezi Septemba mwaka huu.
Kuhusu hali ya mfumuko wa bei katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki alisema alisema mfumuko wa bei wa mwezi Octoba nchini Kenya umeongezeka na kufikia asilimia 6.47 kutoka asilimia 6.34 mwezi septemba mwaka huu, ambapo kwa Uganda mfumuko huo umepungua hadi asilimia 4.1 kutoka asilimia 4.2 mwezi septemba mwaka huu.