Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
OFISI ya Makamu wa Pili wa Rais imeeleza kuwa Dira yake kubwa ni kuwa na Serikali yenye kutoa huduma bora kwa jamii na
yenye muhimili mzuri wa uchumi, umoja na maendeleo endelevu.
Maelezo hayo yametolewa na uongozi wa Ofisi hiyo, wakati wa mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai- Septemba 2012-2013.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd akiwa msimamizi mkuu wa Wizara hiyo alishiriki kikamilifu pamoja na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee nae alishiriki.
Akisoma taarifa ya utangulizi ya utekelezaji wa Malengo makuu hayo ya Wizara, Kaimu Waziri wa Wizara hiyo Ali Juma Shamuhuna alieleza kuwa mbali ya Dira hiyo, pia Ofisi hiyo imeweka dhamira katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali katika sekta zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Pia, Ofisi hiyo ilieleza jinsi inavyoratibu na kusimamia utekelezaji wa mambo ya Muungano kwa kufuata misingi ya Katiba, Sheria na taratibu pamoja na kuhakikisha kufuata misingi ya haki za binaadamu, utawala bora na ushirikishwaji pamoja na kuratibu masuala ya utafiti..
Waziri Shamuhuna alieleza kuwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais imekuwa ikijipangia malengo ya kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA II), Ilani ya Uhaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010-2015 na Malengo ya Milenia.
Alieleza kuwa Ofisi hiyo, imepanga kuwajengea uwezo wafanyakazi wake katika Idara mbali mbali Unguja na Pemba kwa kuwapatia mafunzo, vitendea kazi na kuwaweka katika mazingira bora ya kazi ili kuongeza uwajibikaji, ufanisi na kuleta tija katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi.
Aidha, Waziri Shamuhuna alisema kuwa Ofisi hiyo ilipanga kuratibu shughuli za Baraza la Wawakilishi na kazi za Tume na kusimamia masuala ya utekelezaji wa Mpango wa Kukabiliana na Maafa nchini sanjari na usimamizi na uendeshaji wa masuala ya sherehe na maadhimisho ya kitaifa na kusimamiabaadhi ya changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na uhaba wa wataalamu wa fani muhimu zinazohitajika katika Irada mbalimbali changamoto ambayo hivi sasa inafanyiwa kazi na Ofisi husika.
Sambamba na hayo, Ofisi hiyo ilitoa shukurani kwa Rais pamoja na kuwashukuru Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais na Katibu wwa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkjuu Kiongozi kwa miongozo wanayopewa na kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora chini ya Waziri wake Haji Omar Kheir ambapo Wizara hiyo ilieleza jukumu lake la kusimamia haki na wajibu wa Watumishi wa Umma ili wakuwahudumia wananchi kwa kiwango cha juu na kuleta ufanisi na kuimarisha Utawala Bora nchini.
Aidha, Wizara hiyo ilieleza hatua ilizozifikia za utekelezaji kimalengo ambapo miongoni mwa hizo ni pamoja na kuunganisha taarifa za watumishi wa umma katika mfumo wa malipo ya mishahara pamoja na kuimarisha matumizi ya mfumo wa taarifa za teknolojia ya mawasiliano –ICT.
Wizara hiyo pia, ilianzisha na kuimarisha mipango bora ya upatikanaji wa rasiliamali watu wenye sifa na kuweka mazingira mazuri ya kazi pamoja na kusimamia matumizi mazuri ya fedha katika sekta za umma kwa uwazi na uwajibikaji.
Kuimarisha demokrasia, uwajibikaji, maadili ya viongozi katika utawala na kuzuia rushwa Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi tayari imeshaanza kutumika baada ya Rais kutia saini na kumteua Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, ambapo kumepelekea kuanza rasmi shughuli za taasisi hiyo.
Wizara hiyo pia, ilieleza changamoto kadhaa inazozikabili ambazo hivi sasa zinafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuchelewa kuanza kwa mradi wa e-government ambao kukamilika kwake pia, utasaidia katika kukusanya mapato.
Akitoa shukurani na pongezi zake kwa nyakati tofauti alipokutana na Wizara hizo, Dk. Shein alieleza haja ya kuendeleza ushirikiano katika utendaji wa kazi ili kuzidisha mafanikio yalipatikana.