MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi, baada ya kuumizwa kwenye vurugu zilizotokea Kata ya Makuyuni, Wilaya ya Monduli, Arusha.
Akizungumza mjini hapa jana, Nassari alisema ofisi ya Bunge ndiyo imeamua kumhamishia Muhimbili kutokana na majadiliano na madaktari waliokuwa wakimhudumia Hospitali ya Arusha ya Lutheran Medical Center alipokuwa amelazwa.
“Bunge limegharamia kunisafirisha hadi Muhimbili kwa matibabu zaidi, ofisi ya Bunge ndiyo imetafuta ndege ndogo ya kunipeleka,” alisema Nassari.
Alisema hadi jana alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya mgongo na nyuma ya shingo, ambako alipigwa rungu na vijana wa Kimasai (Morani) na wafuasi wanaodaiwa kuwa wa CCM.
“Baada ya kunipiga nilifanikiwa kutoroka hadi eneo la Minjingu kunusuru maisha yangu, baadaye ilibidi nitafutiwe pikipiki hadi eneo la barabara kuu ndipo niliwakuta askari wa usalama barabarani, waliniombea usafiri hadi hospitali,” alisema Nassari.
Hali tete ya usalama
Katika hatua nyingine, Nassari alieleza kusikitishwa na hatua ya kutaka kuchukuliwa kwa mahojiano mmoja wa majeruhi, ambaye alieleza alimuona mtu aliyetupa bomu kwenye mkutano wa kampeni wa Chadema Juni 15 Uwanja wa Soweto.
“Walikuja polisi kama sita hivi wakimtaka huyu majeruhi, hali ambayo ilizua malumbano hadi nilipongilia kati na nikalazimika kulala naye karibu ili wasimchukue,” alisema Nassari.
Chadema wasafirisha maiti mbili
Licha ya juzi kutokea tafrani ya mabomu Uwanja wa Soweto na kushindwa kuagwa marehemu, watatu waliofariki kutokana na mlipuko wa bomu.
Hata hivyo, Chadema kilifanikiwa kusafirisha maiti mbili; Ramadhan Juma(15) mkazi wa Tabora na Amir Ally(7), mkazi wa Lushoto, mkoani Tanga. Marehemu Judith Moshi (25)ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bawacha Kata ya Sokone 1, anatarajiwa kuzikwa leo.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz