*Asema anatafuta ushaidi mwingine
KIONGOZI Mkuu wa Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), ya mjini The Hague, Louis Moreno Ocampo amesema atawasilisha ushahidi zaidi kutaka mashtaka yathibitishwe dhidi ya Wakenya wawili mashuhuri, ambao majaji katika mahakama hiyo walikataa kuthibitisha mashtaka dhidi yao kuhusiana na ghasia za baada ya uchagzui wa mwaka 2007 nchini Kenya.
Jumatatu hii Mahakama ya ICC ilithibitisha mashtaka dhidi ya washukiwa wanne akiwemo Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta, lakini majaji wakasema hawakuridhishwa na ushahidi uliotolewa na kiongozi wa mashtaka dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Polisi, Major Generali Hussein Ali na Waziri wa zamani, Henry Kosgey, na hivyo kugoma kuthibitisha mashtaka dhidi yao.
Majaji hao waliridhika na ushahidi uliotolewa dhidi ya Mkuu wa Utumishi wa umma. Francis Muthaura, aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu, William Ruto na mtangazaji wa redio, Joshua Arap Sang.
Akihutubia waandishi wa habari katika mahakama ya ICC, Ocampo amesema hatakata rufaa dhidi ya uamuzi wa majaji, lakini ataendelea kukusanya ushahidi zaidi kutoka kwa waathirika na kuwasilisha tena mbele ya jopo la majaji watatu walioshughulikia kesi hiyo ya washukiwa wa ghasia za Kenya ili kuwatia hatiani watuhumiwa walioondolewa.
Amesema atafanya uchunguzi zaidi juu ya, Ali na Kosgey wakati kesi dhidi ya watuhumiwa wanne ambao mashtaka dhidi yao yalithibitishwa itakapoanza. Wakati wa kutoa uamuzi siku ya Jumatatu, jaji kiongozi Ekaterina Trendafilova alisema hawakushawishika na ushahidi uliotolewa wa kumhusisha Kosgey na ghasia dhidi ya wafuasi wa chama cha PNU katika maeneo kadhaa mkoani Rift Valley.
Alielezea kwamba kiongozi wa mashtaka alitegemea shahidi mmoja tu dhidi ya Kosgey, na ambaye hakuthibitishwa. Pia aliongeza kwamba upande wa mashtaka ulibana tarehe ambazo inadaiwa Kosgey alihudhuria mikutano ya kupanga ghasia, na hivyo kumkosesha fursa ya kuandaa utetezi.
Jaji huyo pia alisema ushahidi uliowasilishwa haukuwa na misingi ya kutosha kuonesha kwamba Polisi walishiriki kwenye ghasia katika maeneo ya Nakuru na Naivasha.
Kuhusu uamuzi huo, Ocampo amesema atafanya uchunguzi zaidi katika sehemu za Kisumu na Kibera mjini Nairobi, ambako anadai Polisi walishiriki kwenye ghasia. Amesema atatafuta ushahidi zaidi kuthibitisha kwamba Kosgey alihusika kwenye ghasia pamoja na Ruto na Sang.
-BBC