HALI ya kiafya ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela bado ni kitendawili, baada ya taarifa kueleza kwamba japokuwa ameweza kufungua macho, bado hajitambui na hana uwezo wa kujitegemea kwa chochote.
Taarifa kutoka Afrika Kisini zilieleza jana kwamba hata Rais Jacob Zuma aliingiwa na simanzi na kulazimika kuahirisha safari yake nchini Msumbiji juzi kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa masuala ya uchumi wa kikanda wa Sadc.
Hali ya kiongozi huyo aliyeandika historia kwa kufanikiwa kushinda na kukata minyororo ya ubaguzi wa rangi nchini humo,imeendelea hivyo kwa wiki mbili sasa, ambapo hata Rais Barack Obama aliyewasili nchini humo hatoweza kumuona.
Mandela ambaye amekuwa Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini, hatoweza kuonana na Obama ambaye pia ameweka historia ya kuwa Rais wa Kwanza Mweusi wa Marekani, baada ya kukata minyororo ya kibaguzi iliyokuwa ikiwanyima weusi fursa za kushika nafasi za juu serikalini.
“Lakini, nashukuru kwamba angalau anaonekana kuwa na ahueni,” alisema Zuma akielezea hali ya Mandela anayetarajiwa kutumiza miaka 95 mwezi ujao, ambaye alilazimika kwenda kumwona Mandela hospitali kwa mara ya pili ndani ya saa 24 juzi.
Hata hivyo, mwanawe Makaziwe Mandela alikaririwa jana akieleza kamba anaamini hata pamoja n hali yake kuwa mbaya, lakini baba yake hatakufa kwa sasa kwa kuwa bado mwili wake unaonekana kuwa na nguvu.
“Kila tunapoongea naye anaonekana kutusikia, anafungua macho na kututazama, anatikisa kichwa japokuwa hawezi kujibu lolote.
Ninachotaka ni kueleza kwamba Mungu pekee ndiye anayejua muda anaouhitaji kumchukua,” alisema.
Obama asifia ushujaa wa Mandela
Akizungumza nchini Senegal katika ziara yake juzi, Obama alieleza kuuthamini wasifu wa Mandela na kusema kwamba ni “Shujaa wa kweli”.
“Ni kweli kwamba Mandela ni shujaa wa dunia, na iwapo atafariki na kurejea kwa muumba, ninachoamini ni kwamba urithi aliouachia duniani utaendeela kuenziwa kwa vizazi vyote vijavyo,” alisema
Alieleza namna msimamo wa Mandela ulivyomshawishi kuingia kwenye siasa wakati alipokuwa akipambana dhidi ya ubaguzi wa rangi akiwa shule kwenye miaka ya 1970.
Zuma asikitika, afuta ziara
Juzi, Rais Zuma alifuta ziara yake nchini Msumbiji baada ya kumtembelea Mandela, ambaye amelazwa hospitali ya moyo ya Medi-Clinic mjini Pretoria.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya nchi hiyo imesema, rais Zuma alimtembelea Mandela juzi jioni na kumkuta kiongozi huyo akiwa bado katika hali mbaya, hivyo kumfanya kiongozi huyo kufuta ziara aliyokuwa aifanye Msumbiji.
Akiwa nchini humo, Rais Zuma pia alitarajia kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc), unaohusu uwekezaji kwenye sekta ya miundombinu katika kanda hiyo. Rais Zuma ametoa shukrani kwa niaba ya serikali yake kwa wananchi wa Afrika Kusini ambao wanaendelea kumwombea Mandela.
Pia hali ya usalama imeongezwa katika hospitali alipolazwa kiongozi huyo, na polisi wanaosimamia mageti ya hospitali hiyo wanatumia vifaa maalum kukagua magari kabla hayajaruhusiwa kuingia hospitalini hapo. Mandela alilazwa kwenye Hospitali ya Medi Clinic Heart iliyoko Pretoria kutokana na maambukizi ya homa ya mapafu.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz