Nyota wa mpira wa kikapu Marekani kuja Tanzania

PHARES MAGESA, akizungumza leo

Taarifa kwa wadau na wapenzi wa mpira wa kikapu Tanzania.

SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania pamoja na ndugu zetu wa Ubalozi wa Marekani nchini tuna furaha kubwa leo kwa mara nyingine tena kufanikisha ziara ya kimichezo ya mafunzo ya wachezaji wa zamani wa ligi kubwa ya mpira wa kikapu duniani ya NBA na WNBA.
Miongoni mwa wachezaji wanaokuja katika ziara hii ni Tamika Anderson WNBA, Becky Bonner WNBA na Dee Brown NBA Dallas Maverick, Ni wachezaji walioheshimika sana katika ligi hizo za Marekani.
Kama mnakumbuka mwaka 2008 tulikuwa na ugeni kama huu wa wachezaji wa ligi hizo za Marekani – Matt Boner kutoka San Antonio Spurs na Jennifer Azzi mchezaji wa zamani wa WNBA, All Stars na mshindi wa medali ya dhahabu ambao waliendesha mafunzo kwa vijana chini ya miaka 17 katika viwanja wa Don Bosco Upanga kuanzia tarehe 8 hadi 11 Septemba 2008 ambapo jumla ya vijana 150 kutoka katika shule za Secondari 13 za Jiji la Dar es salaam pamoja na Zanzibar walifaidika.
Kama taarifa ya Bw. Roberto Queroz msafara huo utawasili tarehe 5/9/2011 na wataanza mafunzo tarehe 6/9/2011 hadi tarehe 8/9/2011 katika viwanja vya Don Bosco Upanga na wataondoka Tanzania tarehe 9/9/2011. Kwa upande wetu sisi TBF tayari tumeshaanza maandalizi ya mafunzo haya na hasa mchakato wa kuwapata vijana watakao shiriki katika mafunzo hayakutoka mikoa kadhaa. Mikoa itakayohusika ni pamoja na wenyeji Dar-es-Salaam, Kagera, Mara, Tabora, Mtwara, Ruvuma, Singida, Zanzibar na Pemba, Shinyanga, Kigoma na Iringa ambapo kila mkoa utawakilishwa na vijana 3 na mwalimu 1. Tunatarajia kuwa na takriban vijana 80 katika mafunzo hayo.
Mbali na Kufanya Mafunzo kwa vijana pia wageni wetu hawa watapata nafasi ya kutembelea baadhi ya shule za msingi na secondari na Maeneo mengine ya Jiji la Dar es salaam kujionea baadhi ya vivutio na utamaduni wetu. Maeneo hayo tutawajulisha baadaye.
Kwa kufanikisha program hii, sisi katika TBF na kwa niaba ya wapenzi na wadau wa mpira wa kikapu nchini, tunapenda kuwashukuru kwa dhati kabisa wenzetu wa Ubalozi wa Marekani hususan Balozi
Lenhart pamoja na wafanyakazi wote wa Ubalozi katika kudumisha uhusiano wa kimichezo uliokuwepo baina yetu na watu wa Marekani. Nasi tunawahakikishia kudumisha na kuheshimu mahusiano haya kwa faida ya vijana wetu wa sasa na kizazi kijacho.
Napenda kuwashukuru pia kwa ushirikiano wenu katika kuinua mchezo wa Mpira wa Kikapu na kuweka mshikamano kwa maendeleo ya mchezo wenyewe, familia ya Mpira wa Kikapu inaendelea kutoa rai kwenu kushiriki kikamilifu katika Clinic hii ili kuweza kuutangaza vizuri.
Mwisho napenda kuwakaribisha wapenzi na wadau wote wa mpira wa kikapu – ikiwemo mashirika ya umma, makampuni na hata watu mmoja mmoja kuja kutuunga mkono kwa hali nba mali katika kufanikisha Clinic hii ya Vijana wetu ili nao wajisikie na wapate moyo wa kufika mbali kupitia mchezo wa mpira wa kikapu.
Pia Tunaomba walimu na Wazazi kushirikiana nasi kwa kuwaruhusu vijana watakaokuwa wamechaguliwa kuja kushiriki, tunawahakikishia watakuwa katika mikono salama katika kipindi chote cha mafunzo hayo. Vile vile kwa wale ambao hawakupta nafasi hiyo tunawakaribisha ili waje wajifunze kwa kutazama kwani TBF bado tuna program kadhaa za mafunzo kama haya kwa siku zijazo ambapo wataweza kupata nafasi.
Pia tunapenda kuchukua fursa hii kuwapa taarifa rasmi vyama vya mikoa itakayoshiriki. Ambayo tumeitaja hapo mwanza kuchagua vijana watatu wa umri wa chini ya miaka 16 pamoja na kiongozi/mwalimu mmoja ili washiriki katika clinic hii. Gharama zote ikiwemo nauli, malazi na chakula zitalipwa na TBF. Tupate majina hayo mapema iwezekanavyo. (mikoa)
Nachukua fursa pia kuwataarifu wanakikapu, wapenzi na wadau wote kuwa mwaka huu tutakuwa na matukio mengi ya kitaifa na kimataifa hivyo wajiandae na tutawataarifu kadri muda unavyokwenda.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwatakia wote maandalizi mema ya Mafunzo kwa Vijana na Baraka za Mwenyezi Mungu katika Mfungo Mtukufu wa mwezi wa Ramadhani.
Aksanteni kwa kunisikiliza

Taarifa hii imetolewa na PHARES MAGESA, MAKAMU WA RAIS-TBF