Nyerere Wangu Mimi…!

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere


Nyerere Wangu Mimi!

Na zitto Kabwe

MWAKA 1984 nilianza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kigoma, katika Mji wa Kigoma. Nakumbuka kupelekwa Shule siku ya kwanza na mama yangu mzazi Bi Shida Salum (Mungu amrehemu) nikiwa sina viatu yaani pekupeku wala begi la mkononi, nilikuwa nimebeba mfuko wa nailoni. Nakumbuka usiku wa kuamkia siku ya kwanza kwenda shule, sikulala kwa furaha na hamu ya kuwa msomi, nilijisikia fahari kuanza shule japokuwa sikuwa na kitu chochote cha zaida zaidi ya kaptula ya shule na shati liloshonwa kwa kitambaa cha sanda. Pia nilianza shule nikiwa nimechelewa kwa mwaka mmoja maana wenzangu walianza wakiwa na miaka 7. Mwaka 1983 nilipopelekwa shule mkono wangu haukuweza kushika sikio upande wa pili, ambacho kilikuwa kipimo cha kuandikishwa darasa la kwanza.

Hali ya maisha wakati huo ilikuwa mbaya sana. Nakumbuka kwenda shuleni nikiwa sina kitu tumboni au siku nzima nilikunywa uji usio na sukari. Uji wenyewe ulikuwa ni wa unga wa njano uliotokana na mahindi ya njano ambayo tuliambiwa nchi yetu ililetewa kama msaada kutoka nchini marekani.

Shule yetu kama zilivyokuwa shule nyingi za wakati huo hatukuwa na madawati ya kutosha na vyumba vya madarasa vilikuwa vichache sana. Ilikuwa ni kawaida kwa wadogo (darasa la kwanza mpaka la tatu) kusomea chini ya mwembe na kukaa juu ya matofali. Hali hiyo ilipelekea kaptura yangu ya shule kuwekwa viraka vingi maana ilikuwa inachanika mara kwa mara. Nyakati nyingine ilibidi kwenda shuleni na shati likiwa halijakauka hasa siku za alhamis, siku ya usafi na iwapo nikiwa zamu ya mchana kwani nilikuwa nina shati moja tu tena lililotokana na kitambaa cha sanda.

Kwa dhahiri, watoto wa masikini na matajiri tulikuwa shule moja, darasa moja hata wote kukaa kwenye matofali. Watoto watawala na watawaliwa tulicheza mpira pamoja, kuruka dana na hata kuruka kamba. Hatukujisikia wanyonge kwa sababu hatuna viatu au kuvaa kaptura zenye viraka na mashati ya sanda. Kamwe sikumbuki kudharauliwa shuleni sababu ya uduni wa maisha yangu. Heshima ilitokana na uwezo wako darasani na kupitia hilo nilipata marafiki wa kutoka madaraja yote ya maisha. Nakumbuka mtoto wa Mkurugenzi wa Maendeleo Mkoa wa Kigoma ndugu Daniel Masanja ndiye alikuwa rafiki yangu wa karibu na kwa kuwa sikuwa na hata pesa ya kununua bajia wakati wa mapumziko, yeye alikuwa ananinunulia.

Huko baadaye, ada yangu ya kidato cha kwanza ililipwa na Mzee Sebastian Kasomi ambaye mwanaye Kasomi Mabula alikuwa rafiki yangu mkubwa mara alipohamia shuleni kwetu akitokea mjini Shinyanga. Mzee Kasomi alikuwa Mkuu wa idara ya Kodi ya Mapato mkoani Kigoma.

Licha ya uduni wa maisha watoto wengi tuliishi kwa matumaini makubwa sana. Mwalimu wetu Mkuu ndg. Daniel Andulile alikuwa mkali sana kwa watoto wote bila kujali daraja la maisha la wazazi wao. Alikuwa anatucharaza viboko kwa makosa na utundu bila ubaguzi. Alisisitiza sana kusoma kwa bidii ili kujenga Taifa. Dhana hii ya kujenga Taifa iliingizwa kwenye akili zetu na sisi kumeza bila kujali maana yake. Wakati mwingine tulikuwa tunarudi nyumbani huku tukijadili kitoto kuwa tunajenga Taifa. Kila siku mwendo wa kilometa Sita kwenda na kurudi shuleni.

Elimu hii isiyo ya kibaguzi sasa najua ilitokana na sera za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Jitihada zangu darasani ndio ziilikuwa kipimo cha utu wangu na sio uwezo wa kiuchumi wa wazazi wangu.. Elimu iliyompa fursa sawa za kuendelea na kusonga mbele mtoto aliyekuwa kigoma, kantalamba au Dar es Salaam. Elimu iliyokuza ndoto, kuinua ari na kujenga matumaini ya kila mtoto wa kitanzania. Elimu iliyovunja na kusambaratisha matabaka ya kiuchumi na dhamana. Elimu iliyojenga uzalendo na hamasa ya kutumikia taifa letu kwa misingi ya haki, uadilifu na upendo.

Sikuwahi kukutana na Mwalimu Nyerere isipokuwa niliwahi kumwona akiwa ndani ya gari nikiwa nimepanga mstari barabarani alipofanya ziara mkoani kwetu mwaka 1987 nikiwa darasa la nne. Lakini nilikuwa kama ninaishi naye kutokana na namna nilivyotaka kuwa kama yeye. Nikiwa darasa la pili nakumbuka katika mkebe wangu (mathematical set) mkuu kuu niliweka picha ya kukatwa kutoka kwenye gazeti ya Mwalimu na Kawawa. Na nilijisikia fahari kuwa na picha zao, mara zote nilipokuwa nafungua mkebe kutoa kalamu nilijisemea kimoyomoyo, “siku moja nitakuwa kama wewe”

Licha ya maisha magumu tuliyokuwa tunaishi, maisha ya kupanga mawe kwenye mstari wa kununua mahitaji muhimu kama sukari, sabuni na mafuta kutoka duka la ushirika, maisha ya kushindia uji wa yanga na kutembea mwendo mrefu kwenda shuleni, niliishi kwa imani kubwa kuwa mimi na watoto wengine tupo sawa. Usawa katika kupata elimu, usawa katika kucheza na usawa katika ndoto na matumaini. Nimemaliza elimu ya Chuo Kikuu, ndoto niliyoruhusiwa kuwa nayo kwa sababu ya sera za Ujamaa, za Mwalimu Nyerere.

Ujamaa haukuwa katika usawa wa elimu tu ambapo kila mtoto alipata elimu bure na bora katika Shule za umma bila ubaguzi bali pia namna jamii iliishi. Mtoto alikuwa analelewa na jamii nzima. Ukifanya makosa mtaani mzazi yeyote anakuadhibu ili kukurekebisha. Ukifanya jambo jema, mzazi yeyote anakupongeza.

Mwaka 1985 mwezi Novemba nilipokuwa natoka shuleni, karibia na Benki ya Taifa ya Biashara Tawi la Obed Katikaza, nilikutana na Mama Colleta Furugunya tuliyekuwa tunaishi mtaa mmoja na nikimwita bibi Colleta. Aliponiuliza matokeo yangu ya mtihani wa kumaliza muhula wa pili wa darasa la pili kwa kujiamini nikampa karatasi yangu ya matokeo. Nilikuwa nimeshika nafasi ya tatu darasani nyuma ya Ramadhan Kalukula na Haki Manyaga.

Bibi Colleta alinishika mkono mpaka duka la Viatu, Bora Shoes na kuninunulia jozi yangu ya kwanza ya viatu. Viatu vile viliitwa Asante Salim, aliyekuwa Waziri Mkuu wa mwisho wa Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa anajaribu kubadili hali mbaya iliyokuwepo. Hivyo ndivyo nilivyopata viatu vyangu vya kwanza vya shule. Shukrani kwa sera nzuri ya ujamaa, mshikamano na upendo.

Hizo ni enzi.