RAIS wa Rwanda Paul Kagame amesema kuwa atataoa masaada wa haraka kumsafirisha mshukiwa wa uhalifu wa kivita nchini DRC Bosco Ntaganda kwa mahakama ya kimataifa ya jinai, (ICC).
Mshukiwa huyo anayejulikana kama “The Terminator”, alijisalimisha kwa ubalozi wa Marekani, Rwanda, Jumatatu. .
Rais Kagame amesema kuwa Rwanda itawezesha kusafirishwa kwa mshukiwa huyo hadi Hague haraka iwezekanavyo.
Generali Ntaganda amekuwa mhusika mkubwa katika mzozo wa mashariki ya DRC.
ICC imeshtaki kwa makosa kumi ya uhalifu wa kivita, dhuluma dhidi ya ubinadamu na kumtuhumu kuwaingiza watoto wadogo kwa jeshi lake, kuwafanya wanawake kuwa watumwa wa ngono na kuhusika katika mauji ya watu mia nane katika miaka ya 2002 na 2003.
Hata hivyo Generali Ntaganda amekanusha mashtaka hayo. .
Kadhalika amekuwa mpiganaji wa makundi kadhaa ya waasi na vile vile jeshi la Congo katika nchi ambayo imegawanyika kikabila na kung’ang’ania rasilimali zake za madini.
Hivi karibuni inaaminika kuwa alikuwa mmoja wa viongozi wa kundi la wapiganaji la M23, ambalo linapigana na jeshi la serikali katika sehemu ya mashariki.
Kadhalika amepigania jeshi la Rwanda ambayo imekanusha madai ya Umoja wa mataifa kuwa inafadhili wapiganaji wa M23.
Katika taarifa Kagame amesema kuwa “Tutashirikiana na ubalozi wa Marekani kuhusiana na kesi na Ntaganda haraka iwezekanavyo,”
Matamshi hayo yanajiri siku moja tu baada ya naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayeshughulikia Afrika ,Johnny Carson, kusema kuwa ni muhimu safari ya Generali Ntaganda kutoka katika ubalozi hadi uwanja wa ndege isivurugwe.
Balozi Carson amesema kuwa anatumaini kuwa maafisa wa ICC wako safarini kuelekea Rwanda na wataruhusiwa katika nchi hiyo. Rwanda na Marekani zote si nchi wanachama wa ICC
Jumatano mwendesha mkuu wa mashtaka Fatou Bensouda, amesema kuwa anatarajia Generali Ntaganda kuwasilishwa katika mahakama hiyo katika siku chache zijazo.
Mahakama ya ICC ilikuwa imetoa kibali cha kumkamata Ntaganda miaka saba iliyopita.
Serikali ya DRC ilisema kuwa Generali Ntaganda, anayetoka katika kabila la Watutsi aliingia ndani ya Rwanda Jumamosi baada ya yeye na baadhi ya wafuasi wake kushindwa na kundi pinzani ndani ya M23.
Rwanda imekanusha kumsaidia Generali Ntaganda kutoroka DRC ama kupanga ajisalimishe kwa ubalozi wa Marekani ambao unapakana na wizara ya ulinzi huko Kigali.
Kadhalika serikali ya Rwanda ina watutsi wengi ambao Generali Ntaganda alipigana nao wakiwa waasi lakini sasa wako madarakani.
-BBC