Na Joachim Mushi
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Temeke limefanya semina kwa maofisa ajira na Fedha zaidi ya 150 kutoka katika makampuni na taasisi anuai za eneo hilo ikiwa ni jitihada za kutoa elimu juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo.
Semina hiyo iliyofunguliwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Cresentius Magori imefanyika leo jijini Dar es Salaam, ambapo washiriki mbali na kupewa elimu juu ya mafao saba yanayotolewa na shirika hilo pia wameelezwa namna ya mfumo mpya wa ukokotoaji mafao kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).
Akifungua semina hiyo Mkurugenzi Uendeshaji wa NSSF, Cresentius Magori aliwataka washiriki kuitumia vizuri elimu watakayoipata juu ya shughuli za shirika hilo ikiwemo kuwaelimisha wafanyakazi umuhimu wa mafao mbalimbali yanayotolewa na NSSF ili waweze kuzitumia vema fursa zilizopo katika mafao hayo.
Alisema wapo baadhi ya wafanyakazi ambao hukimbilia kujitoa mara baada ya kuacha kazi jambo ambalo alieleza lina athari kubwa kwao hapo baadaye kwani kitendo cha kujitoa mara kwa mara huenda kikamkosesha sifa za kupata mafao hapo baadaye.
“Fao la kujitoa lipo…lakini hii kitu ya kujitoa sio nzuri maana inaweza kumkosesha mwanachama kupata penseni hapo baadae. Maana ili mwanachama apate pensheni kuna idadi ya michango ambayo inatakiwa awe ametimiza…sasa kama ataendelea kujiunga na kujitoa anaweza asifikishe,” alisema Magori.
Aidha alisema wapo baadhi ya wafanyakazi wamefikia hatua ya kugushi barua kuwa wameacha kazi ili wachukue michango yao jambo ambalo ni hatari na kinyume cha sheria, hivyo kuwataka maofisa ajira hao kuwa makini na mchezo huo mbaya kwani unaweza kuwaingiza matatizoni endapo watabainika kushiriki ulaghai huo.
Akizungumzia uhai wa NSSF aliwahakikishia wanasemina hao kuwa shirika hilo lipo salama kutokana na mafanikio na mikakati iliyonayo hivyo wasidanganyike na taarifa zozote zisizo rasmi ambazo wakati mwingine zimekuwa zikiwaongopea wananchini.
“…Mfuko wetu upo salama na imara hatujafilisika na hatuwezi kufilisika, maana kwa ukaguzi ambao ulifanywa hivi karibuni unaonesha shirika liposalama kwa miaka 50 ijayo sasa tutafilisika kwa vipi? Bado tumekuwa wa kwanza kimataifa kufanya vizuri kiutendaji kadri ya tulivyojipangia katika utoaji huduma na huduma zimeboreshwa,” alisema Magori.
Kwa upande wake Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke, Yahya Mhamali alisema licha ya uboreshaji wa huduma ndani ya shirika hilo kwa sasa mtu atakayemshawishi mteja/wateja wapya kujiunga na mfuko huo atapata asilimia 10 ya mchango wao wa kwanza mara baada ya kuanza kuchangia ikiwa ni kama asante kwake.
“…Hii sio rushwa maana sisi kila siku tunazunguka kushawishi wananchi kujiunga na mfuko wetu sasa kama wewe umetusaidia na mwanachama akaja kwetu kwanini tusikupe asante? Maana hapa umelisaidia taifa kwa mwanachama huyu kuingia katika eneo salama kwa maisha yake ya baadae,” alisema Mhamali.
Akitoa ufafanuzi katika mada yake kwa wanasemina, Meneja Mafao Mkoa wa Temeke, James Oigo alisema NSSF kwa sasa inaendelea kutoa mikopo kwa wanachama wake kupitia Saccos mbalimbali ikiwa ni hatua ya kuwajali wanachama wake hivyo kuwashauri wanachama kutumia fursa hiyo kujiletea maendeleo kwa kupata mikopo iliyo na riba nafuu.