NSSF yajitosa Kiwira

  • *Yaomba ikabidhiwe mgodi izalishe umeme megawati 500
  • *Italipa madeni ya bilioni 28/-, mishahara ya watumishi wote
  • *Tanpower kikwazo kwa hisa 70%, wizara yaweka kauzibe
  • *Zito: Mkopo wa kujenga nyumba za Jeshi usitumiwe Kiwira

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limejitosa katika mradi mkubwa wa kuzalisha umeme nchini kwa kuonyesha nia ya kununua Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira.

Uamuzi huu wa NSSF, utawalazimu kulipa deni linaloikabili Kiwira la wastani wa Sh bilioni 28, lakini pia utalisaidia taifa kupata megawati 500 mpya kwenye gridi ya umeme ya taifa ndani ya miaka mitano.

NSSF wamefikia uamuzi huo, baada ya Mgodi wa Kiwira Coal and Power Limited, kuwa wamechukua mkopo wenye thamani ya dola milioni 7.0 (Sh bilioni 9.009) kutoka kwa shirika hilo mwaka 2007, na kushindwa kulipa deni.

Historia ya Mkopo

Mwezi Julai, 2005, Kampuni ya Tanpower Resources pamoja na Serikali waliungana na kuunda kampuni iitwayo Kiwira Coal and Power Limited (KCPL). Katika Kampuni hii, Tanpower Resources ina hisa 700,000 na Serikali ina hisa 120,000. Kampuni hii (KCPL) iliundwa ili kuendesha mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira na Ilima. Umiliki huu ni wastani wa asilimia 70 KCPL na 30 kwa Serikali.

Mgodi wa Kiwira una uwezo wa kuzalisha tani 150,000 za makaa ya mawe kwa mwaka na mgodi wa Ilima una uwezo wa kuzalisha tani 15,000 kwa mwaka. Mwishoni mwa mwezi Desemba 2005, Kampuni ya Tanpower Resources yenyewe ilinunua mgodi wa Kabulo wenye uwezo wa kutoa tani milioni 100 za makaa ya mawe. Mgodi wa Kabula upo pembeni ya mgodi wa Kiwira.

Mwezi Aprili 2007 Kampuni ya Kiwira Coal and Power Limited (KCPL) iliomba mkopo wa muda mfupi kutoka NSSF. Mkopo huo wa Dola za Kimarekani milioni 7 (sawa na Sh 9,009,000,000) ulikuwa kwa ajili ya kulipia malipo ya awali ya kununulia mitambo na mashine kutoka China kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe na umeme. Mkopo huu ulikuwa urudishwe katika kipindi kisichozidi miezi sita. Fedha za kulipia mkopo huu zilikuwa zitokane na mkopo ambao ungetolewa na benki nyingine ambazo zilikuwa zinaongozwa na Benki ya CRDB.

Katika kikao maalum cha 45 kilichofanyika tarehe 29 April, 2007, Bodi ya Wadhamini ya NSSF iliridhia Shirika kutoa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 7 kwa Kampuni ya Kiwira Coal and Power Limited (KCPL) kwa ajili ya mradi wa kuzalisha umeme. Mkopo huo ulipotolewa Julai, 2007 ulikuwa sehemu ya mkopo ambao ulitolewa na taasisi tatu za fedha. Taasisi nyingine zilizotoa mkopo ni Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) na Benki ya CRDB

Mkopo uliotolewa na NSSF ulidhaminiwa na Benki ya CRDB. Benki hii ilidhamini mkopo huu baada ya kupata dhamana ya Serikali kupitia Benki Kuu.

Benki ya CRDB kwa kushirikiana na taasisi nyingine za fedha ilipewa jukumu na kampuni ya KCPL kutafuta mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 93. Mkopo huo ulitegemewa utolewe na taasisi za fedha ambazo ni kampuni zinazomilikiwa na Serikali ya China, Benki ya CRDB, Benki ya PTA, EADB, DBSA, Benki ya Stanbic (T) Ltd, Rand Merchenat na IFC.

Mkopo huo ulikuwa utumike kuzalisha umeme wa Megawati 50. Kati ya fedha hizo, kiasi cha Dola za Kimarekani millioni 7 zilikuwa kwa ajili ya kulipia mkopo uliotolewa na NSSF.

Muda wa mkopo wa NSSF ulikuwa wa miezi sita ambayo iliisha Januari 8, 2008. Kampuni ya KCPL ilishindwa kulipa mkopo huo kwa sababu ya kushindwa kupata mkopo wa Dola za Kimarekani millioni 93 ambazo zilikuwa zitolewe na taasisi nyingine za fedha zilizotajwa hapo juu.

Kwa muda wote huo, NSSF imefanya juhudi kuhakikisha inalipwa fedha zake na kampuni ya KCPL, bila mafanikio.

Jinsi walivyodai mkopo

Mkopo uliotolewa na NSSF unatozwa riba ya asilimia 18.51 kwa mwaka. Hadi kufikia Januari 31, 2011, jumla ya riba ilifikia Sh milioni 6,285.95 na kufanya jumla ya deni la NSSF kwa KCPL kuwa Sh 15,449,647,527.29. Ukichukua mikopo iliyotolewa na Benki ya CRDB na PSPF kwa KCPL pia, jumla ya deni lote ni Sh 28,869,938,996.99 kama linavyooneshwa kwenye Jedwali hapa chini.

Jendwali Na 1: Jumla ya mkopo kwa KCPL hadi kufikia 30, Desemba 2010
Mkopeshaji Mkopo uliotolewa Mkopo uliobaki Riba Jumla ya Deni na Riba
NSSF 9,009,000,000.00 9,009,000,000.00 6,285,946,801.01 15,294,946,801.01
PSPF 5,421,551,370.00 5,421,551,370.00 4,076,020,973.70 9,497,572,343.56
CRDB 2,508,000,000.00 2,490,000,000.00 1,587,419,851.92 4,077,419,851.92
Jumla 16,938,551,370.00 16,920,551,369.86 11,949,387,626.63 28,869,938,996.49

NSSF mara kwa mara wamefanya mawasiliano na majadiliano na CRDB na KCPL kuhusiana na deni bila mafanikio.

Kutokana na KCPL kushindwa kulipa deni lake, Julai, 2009 CRDB (kama mdhamini) ilimwandikia Waziri wa Nishati na Madini kuomba Serikali kulipa mkopo kwa kuwa ndiye Mdhamini Mkuu wa mkopo huo.

Septemba 5, 2009, Waziri alijibu barua iliyoandindikwa na CRDB, na kuahidi kuwa Wizara ingefanya kazi kwa kushirikiana na wakopeshaji kuhakikisha suala hilo linatatuliwa mapema iwezekanavyo.

Baada ya kimya cha muda mrefu, mwezi Februari 2010, CRDB ilimkumbusha Waziri kuhusiana na kushindwa kwa KCPL kulipa deni lake. Benki hiyo ilieleza kuwa hatua iliyobaki ni kwa wakopeshaji kuuza mgodi wa KCPL kwa mnunuzi yeyote kurudisha fedha walizoikopesha KCPL.

Wizara iliendelea kukaa kimya kwa muda wa miezi 10. Desemba 2010, Benki ya CRDB ilituma barua nyingine kwa Waziri wa Nishati na Madini ikimtaarifu kwamba wakopeshaji hawana njia nyingine zaidi ya kuuza Mgodi wa Kiwira. Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya Olympic Exploration kuelezea mahitaji yao ya kununua KCPL.

NSSF kuchukua Kiwira

Kwa hali halisi kama iliyoelezwa hapo juu, NSSF iliona kwamba ili kuokoa mgodi wa Kiwira na kwa maslahi ya umma, ni bora ipewe mgodi huo itafute mbia (Strategic Investor) na kuwekeza katika kuzalisha umeme ambao hatimaye utauzwa kwa TANESCO.

Desemba 8, 2010, NSSF iliandika barua ya kupendekeza/kuomba Serikali kuruhusu NSSF kupewa mgodi wa Kiwira kwa thamani ya dola moja (1) ya Kimarekani. NSSF ilionyesha utayari wa kuwalipa wadeni wengine wa Kiwira ambao ni CRDB na PSPF na madeni mengine yoyote hasa madeni ya mishahara ya wafanyakazi.

Baada ya kupokea barua kutoka NSSF, Consolidated Holding Corporation (CHC) iliiandikia NSSF kuomba kukutana nayo kuwasilisha pendekezo lake juu ya ununuzi wa KCPL. Pendekezo la NSSF liliwasilishwa CHC Makao Makuu Desemba 22, 2010 katika kikao kilihudhuriwa na wajumbe kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, STAMICO, na Mamlaka ya udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).

NSSF iliandika barua mbili, moja kwa Benki ya CRDB kutoa ushauri wa kuahirisha mchakato wa kuuza Kiwira na ya pili kwa Mkurugenzi Mkuu wa Consolidated Holding Corporation kuweka kumbukumbu ya makubaliano yaliyoafikiwa katika kikao hicho kusaidia katika utoaji wa maamuzi juu ya suala hili.

Katika barua ya CHC, NSSF walisisitiza kuwa ni muhimu Serikali kuingiza na kuikabidhi NSSF Mgodi wa Kabulo ambao ulinunuliwa na Kampuni ya Tanpower Resources kuwezesha uzalishaji wa Megawati 500 za umeme. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mgodi wa Kabulo haumilikiwi na KCPL.

Januari 6, 2010, CHC iliandika barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi kumtaarifa juu ya mapendekezo yaliyofikiwa na Kamati ya Ufundi ya Ubinafsishaji (DTT) kuhusu pendekezo la NSSF kupatiwa mgodi wa Kiwira.

NSSF ilivyojipanga ikipewa Kiwira

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa NSSF, Yacoub Kidula, NSSF imejipanga kutekeleza mradi huu katika hatua kadhaa na kwa sasa fedha za utekelezaji zipo wala hawaendi kuzitafuta popote. Hatua ya kwanza katika utekelezaji ni kwa NSSF kupokea mradi kutoka Serikalini na kutafuta mbia (Strategic Investor). Mchakato mzima hadi kuanza utekelezaji wa mradi unategemewa kuchukua miezi mitano kuanzia mwezi Machi, 2011. Mradi huu umegawanywa katika miradi midogo minne.

Mradi wa Kwanza

Hii itahusisha ufufuaji wa awali wa mgodi wa Kiwira. Utafiti mpya wa mgodi wa makaa ya mawe na uhakiki wa usalama wa paa la chini ya ardhi la mgodi.

Katika hatua hii wataajiri watendaji kama mafundi, wasimamizi, wafanyakazi wenye ujuzi na wahudumu. Inatarajiwa kwamba mradi huo utakamilika ndani ya miezi sita tangu siku Serikali itakapokabidhi mradi huo kwa NSSF.
Mradi wa Pili
Anasema katika hatua hii watafanya ufufuaji wa mitambo ya uzalishaji wa umeme na kubadilishwa kwa boilers zilizopo na ununuzi wa vipuri na vifaa vingine. Watumishi wengine wa Ufundi, wataalam na wahudumu. Miradi yote miwili itafanyika sambamba na itamalizika ndani ya miezi sita.

Mradi wa Tatu

Kidula anasema wa mtambo wa kwanza wa kuzalisha Megawati 200 za umeme utaanzishwa. Hatua hii inahusisha upatikanaji wa kumbukumbu muhimu, michoro n.k. Pia watanunua mtambo mpya wa kuzalisha umeme. Mradi huu unategemewa kuanza mwezi Julai, 2012 na utakamilika kati ya miaka miwili na mitatu.

Mradi wa Nne

Anasema mtambo wa kuzalisha Megawati 300 za umeme harakati zake zitaanza rasmi katika hatua hii. Hii itahusisha kukamilisha Mchanganuo wa Biashara na upatikanaji wa mtaji. Utekelezaji na ajira ya timu ya maafisa wa kiufundi wataajiriwa kwa ajili upatikanaji wa mtambo wa kuzalisha Megawati 300 za umeme zilizobaki. Mradi huu unategemewa kuanza mwaka 2016 na kukamilika mwaka 2018.

Faida

NSSF wanasema hatua hii ya kuimiliki na kuiendesha Kiwira itakuwa faida ya pekee kwani utakuwa unaendeshwa na taasisi ya umma na hivyo kumilikiwa na Watanzania kwa ujumla. Mgodi huo utatoa ajira kwa wafanyakazi wa sasa 419 na wafanyakazi wapya ambao wataajiriwa 1,000.
Makaa ya mawe yatazalishwa kuuzwa ndani na baadhi kuuzwa nje ya nchi na hivyo kuliingizia taifa pato la fedha za kigeni; na mwisho mradi wa umeme utapunguza kasi ya mgawo wa umeme unaolikabili taifa kwa sasa.

CHC yaonyesha nia

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Consolidated Holding Corporation, Methusela Mbajo, alisema baada ya vikao vilivyovanywa, wanaangalia uwezekano wa kuwaandikia barua ya muda NSSF waweze kuanza kazi ya kuzalisha umeme wakati majadiliano mengine yakiendelea.

Mbajo alisema CHC inafanya ukaguzi wa mali za Kiwira kwa sasa, ambao utaiwezesha kujua thamani halisi ya Kiwira kabla ya kuirejesha hisa za Tanpower resources na kukabidhi mgodi huo kwa mwekezaji mpya.

Tanpower Resources kikwazo

Hadi sasa umiliki wa mgodi wa Kiwira wenye madeni makubwa kiasi hicho, unamilikiwa kwa ubia wa asilimia 70 kwa Tanpower Resources na Serikali asilimia 30. Majadiliano ya aina yoyote yanapaswa kufanywa, ambayo yataiwezesha Tanpower Resources ama kulingana na madeni yaliyopo au kwa njia nyingine kurejesha hisa zake serikalini kwani imeshindwa kuundesha mgodi huo.

Ingawa hawajatoa kauli rasmi, kwa muda wa karibu miezi 18 sasa Serikali imekuwa ikilipa mishahara ya wafanyakazi. Hakuna kinachoendelea kwani hakuna kinachozalishwa na wafanyakazi wamebaki kuwa walinzi wa mgodi huo, hivyo kwa hali yoyote inapendekezwa kuwa Tanpower Resources irejeshe haraka hisa zake serikalini ziweze kumilikishwa kwa NSSF izalishe umeme.

Uchakavu wa miundombinu

Kikwazo kikubwa kinachojitokeza sasa, ni kwamba umeme utakaozalishwa katika mikoa ya kusini ni mkubwa kuliko uwezo wa mfumo wa kuzalisha umeme uliopo. Kwa mfano, NSSF wakizalisha hizo megawati 500, njia ya kusafirisha umeme iliopo kwenye gridi ya taifa ni msongo wa kilovoti 220, wakati unahitajika msongo wa kilovoti 400 ndipo umeme huo uweze kupokelewa.

Serikali ya Japan kwa kushirikiana na wahisani wengine, tayari imekwishatoa mkopo kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ambapo unakadriwa kufikia dola milioni 250, utakaotumika kujenga msongo wa kilovoti 400 kutoka Shinyanga hadi Iringa.

Wakati ukiwapo mpango huo, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), kwa mujibu wa Mwenyekiti wake, Dk. Chrisant Mzindakaya, lina mpango wa kuzalisha megawati 600, ambapo nao wanataka msongo wa umeme upanuliwe na kufikia kilovoti 400 badala ya 220.

Wawekezaji hawa kutoka China watakaoshirikiana na NDC huko Mchuchuma, wanapanga kuwekeza wastani wa dola bilioni 3.5, ambapo kwa pamoja watazalisha umeme na kutengeneza kiwanda cha kuzalisha chuma huko Liganga.

Watajenga msongo wa kilovoti 400 kutoka Mchuchuma hadi Mufindi, ambapo wanaomba Serikali ijenge kipande cha Mufindi hadi Iringa Mjini, kuunga msongo wa kilovoti 400 kutoka Kusini hadi Shinyanga. Mgodi mwingine wa Ngaka, wanapanga kuzalisha megawati 400.

Kwa mipango hii, ni wazi ndani ya muda wa miaka mitacho kupitia migodi ya Kiwira (megawati 500), Mchuchuma (megawati 600) na Ngaka (megawati 400), ndani ya miaka mitano nchi itapata megawati 1500 ndani ya miaka mitano.

Mkopo wa Exim Bank

Hata hivyo, inaelezwa kuwa kuna mchezo wa danadana unaochezwa serikalini na hasa Wizara ya Nishati na Madini, ambapo waliomba mkopo kutoka Benki ya Exim ya China tangu mwaka 2006 kwa nia ya kuendeleza Kiwira, hawakupata majibu hadi miaka mitano baadae. Wiki iliyopita, baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kwenye hotuba yake kuwa kuna mkopo kutoka China, ndipo wamekuja wawekezaji kutoka China, waliodai wanataka kuikopesha Kiwira dola milioni 450 ianze tena biashara.

Nyumba za wanajeshi

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zito Kabwe, anasema Serikali inataka kutumia mkopo ulitolewa na China kujenga nyumba za wanajeshi kuwekeza Kiwira. “Hatuwezi kuliingiza taifa kwenye mikopo wakati wapo strategic investor kama NSSF wenye uwezo wa kuwekeza Kiwira.

“Serikali imeshindwa kubadili umiliki toka 2009 sasa hivi wanaleta Wachina, kulipotezea muda taifa. Nasema wanajeshi wetu wana haki ya kujengewa nyumba, hivyo mkopo huo usibadilishwe matumizi. Kiwira wapewe wazawa mambo yaende haraka,” alisema Zito jana.

Wiki iliyopita, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma ilitembeleza migodi ya Mchuchuma, Kiwira na Ngaka, ambapo ilishuhudia maandalizi kemkem ya kulinusuru taifa na mgawo wa umeme, ingawa kuna dalili kuwa baadhi ya watendaji wizarani wanataka kuchelewesha kasi ya upatikanaji wa umeme kwa kuwapiga danadana wawekezaji wa ndani.