NSSF Yaisimamisha Sekretarieti ya NSSF Media Cup

Wachezaji wa timu ya Netball ya NSSF wakimsikiliza mgeni rasmi Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga.

Wachezaji wa timu ya Netball ya NSSF wakimsikiliza mgeni rasmi Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga.

NSSF Media Cup, Bonanza, Dar

BAADA ya kuenguliwa kwa timu tano za vyombo vya habari vya Global, Changamoto, Business Times, Radio Maria na New Habari kutokana na kuchelewa kuwasilisha majina ya wachezaji kwenye usajili, ikiwa ni mara ya kwanza katika miaka 12 tatizo kama hili kutokea, NSSF iliona ni vyema kutengua kanuni hii na kuweka adhabu itakayotosha kosa hili, na kurudisha timu hizi tano za vyombo vya habari kushiriki michezo hii ya kirafiki.

Hivyo basi, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii ( NSSF) ilirejea kwenye sekretarieti kuiomba itengue uamuzi huo na kurudisha timu hizi ili kuendeleza ushirikiano na mshikamano kati ya Shirika na Vyombo vya Habari.

Sekretarieti kwa kupitia viongozi wake, Mwenyekiti na Katibu wamekataa kabisa kukubali maombi ya NSSF ambao ndio wenye mamlaka na michezo hii ya kirafiki. Kutokana na hili kumekuwa na malalamimo mengi kutoka kwa vyombo vilivyoenguliwa kushiriki.

Shirika linatambua kuwa bila kutafuta suluhisho la changamoto hii, azma ya kujenga uhusiano baina yake na media haitafikiwa. Hivyo basi, kutokana na mgongano huu wa kimamlaka kati ya NSSF na Sekretarieti ya usimamizi ya michezo hii, NSSF imeamua kusitisha uongozi wa Sekretarieti rasmi kuanzia
tarehe 13 Machi 2015.

NSSF imechukua tena usimamizi wa mechi hizi za kirafiki mpaka Jumatatu tarehe 16 Machi 2015 itakapotangaza Uongozi mpya kusimamia michezo hii. Aidha kamati hii mpya itasimamia utengenezaji wa kanuni mpya ili kulinda azma ya michezo hii ya kirafiki pamoja na kuleta kanuni zitakazoboresha usajili kwa mechi za mwaka ujao.

Timu hizi tano zimerudishwa rasmi leo tarehe 13 Machi 2015 na zitashiriki kuanzia Jumatatu tarehe 16 Machi 2015 kwa mujibu wa ratiba mpya iliyoambatanishwa. Tunawashukuru sana kwa ushirikiano wenu. Na tunaomba radhi kwa usumbufu uliotokea. Ratiba mpya itatangazwa Jumapili 14 Machi 2015.
IMETOLEWA NA IDARA YA MASOKO NA UHUSIANO, NSSF