NSSF sasa kuzalisha umeme nchini

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF (kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo, Abubakar Rajab.

Na Joachim Mushi

Mwanza

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limesema litaanza kuzalisha umeme muda mfupi baadaye na kuliuzia Shirika la Ugavi wa Umeme nchini ili kuchangia kupunguza kero ya nishati hiyo nchini, inayoendelea hapa nchini.

NSSF imesema tayari imemuweka mkandarasi ambaye anafanya utafiti wa kitaalamu kuangalia ni eneo gani linafaa kufungwa mitambo ya shirika hilo itakayozalisha umeme nchini kukabiliana na kero ya takribani miaka yote ya uzalishaji umeme wa uhakika.

Hayo yalibainishwa juzi mjini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Ramadhan Dau alipokuwa akifanya mahojiano na Jambo Leo katika ziara yake na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa NSSF, kutembelea miradi mbalimbali ya shirika hilo Mwanza na Bukoba.

Dau alisema kwa sasa shirika hilo litafunga mitambo ya kufua umeme wa megawati 300, ambayo wamekusudia kuifunga kati ya eneo la Dar es Salaam, Mkuranga na Somanga.

Aidha alisema kabla ya Desemba mwaka huu mchakato utakuwa umeanza wa kukamilisha adhma hiyo ya kuanza kuzalisha nishati ya umeme nchini. NSSF imekuwa ikiwekeza maeneo mbalimbali katika shughuli za kijamii miradi ambayo imekuwa ikifanya vizuri na kutoa mchango mkubwa wa kimaendeleo.

“Kazi hiyo inakwenda vizuri tayari tumeweka mkandarasi ambaye anafanya kazi ya kiupembuzi kuangalia ni eneo gani tuweke mitambo hiyo ya kufua umeme, kati ya Dar es Salaam, Mkuranga na Somanga,” alisema Dau katika mahojiano.

Akizungumzia shirika hilo kuanza kuzalisha umeme wa makaa ya mawe ya Kiwira, Dau alisema NSSF ipo tayari kuanza kufanya kazi hiyo na inachosubiri kwa sasa ni kukabidhiwa mradi huo rasmi wa makaa ya mawe ili waanze kazi.

“Kwa hilo sisi tupo tayari kuanza kazi tunachongojea ni kukabidhiwa mradi huo wa makaa ya mawe. Tukisha pata kibali hakuna kikwazo tunaanza kazi,” alisema Dau.

Akizungumzia mradi wa ujezi wa daraja la Kigamboni ambao utajengwa na NSSF kwa mkopo dhidi ya Serikali alisema maandalizi yanaenda vizuri na kazi ya sasa inayofanyika ni kuandaa michoro ya daraja hilo.

“Mradi huu wa daraja unaenda vizuri, sasa kinachofanyika ni kukamilisha michoro…,” alisema Mkurugenzi huyo Mkuu wa NSSF.

Mwisho