Nsajigwa aumia mazoezini, wachezaji wa kulipwa waanza kuwasili

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

Na Mwandishi Wetu

NAHODHA wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa ameumia nyonga (groin) kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika leo Oktoba 3 mwaka huu, kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa daktari wa Taifa Stars, Dk. Mwanandi Mwankemwa, maumivu hayo yatamweka Nsajigwa ambaye pia ni Nahodha wa Yanga nje ya uwanja kwa kati ya wiki mbili hadi nne.

Kutokana na ushauri wa daktari, Kocha Jan Poulsen amemuondoa kwenye kikosi hicho ambacho kitasafiri Oktoba 6 mwaka huu kwenda Casablanca, Morocco kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Oktoba 9.

Badala yake Kocha Poulsen amemuita kwenye timu yake Nassoro Masoud Said ‘Cholo’ wa Simba kuziba nafasi ya beki huyo wa pembeni.

Wakati huo huo, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema wachezaji wanaocheza nje ya nchi walioitwa na Kocha Poulsen wameanza kuwasili. Katika taarifa yake Wambura aliwataja wachezaji waliowasili hadi sasa ni Idrissa Rajab anayechezea Sofapaka ya Kenya na Mbwana Samata wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kuongeza kuwa waliwasili jana jioni na tayari wameripoti kambini Taifa Stars.

“Henry Joseph wa Kongsvinger IL ya Norway), Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada) na Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden) wanatarajiwa kuwasili leo (Oktoba 3 mwaka huu) usiku kwa ndege ya KLM.
Washambuliaji Abdi Kassim na Dan Mrwanda wanaochezea timu ya DT Long An ya Vietnam ndiyo watakaokuwa wa mwisho kujiunga na kambi ya Stars ambapo watawasili nchini kesho (Oktoba 4 mwaka huu) saa 7 mchana kwa ndege ya Qatar Airways,” alisema Wambura.