NMB Yazinduwa Kituo cha Biashara Mkoa wa Mbeya…!

Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bi Ineke Bussemaker akiwakaribisha wafanyabiashara waliofika katika uzinduzi wa NMB Business Center Jijini Mbeya

Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bi Ineke Bussemaker akiwakaribisha wafanyabiashara waliofika katika uzinduzi wa NMB Business Center Jijini Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abbas Kandoro alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa NMB Business Center Mkoa wa Mbeya akizungumza na wafanyabiashara katika uzinduzi huo
Mkuu wa Idara ya Biashara Bw. James Meitaron akimfafanulia jambo Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bi. Ineke Bussemaker. Anaeshuhudia katikati ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi wa benki hiyo Bw. Abdulmajid Nsekela.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa kituo cha biashara cha NMB (NMB BUSINESS CENTER) Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abbas Kandoro akizungumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bi. Ineke Bussemaker na Afisa Mkuu wa Huduma kwa Wateja Binafsi Bw. Abdulmajid Nsekela katika uzinduzi wa kituo hicho hivi karibuni.
Meneja wa NMB Business Center Jijini Mbeya Bi. Mary Ngalawa akimuonyesha Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bi. Ineke Bussemaker maeneo mbalimbali ya kituo hicho.
Benki ya NMB imezindua kituo cha biashara (NMB BUSSINESS CENTER) mkoani Mbeya kitakachokuwa kikihudumia wateja wafanyabiashara na kuboresha uendeshaji wa biashara kwa wateja wafanyabiashara katika Mkoa huo.
Akiongea katika uzinduzi wa kituo hicho Afisa Mkuu wa wateja binafsi wa NMB Abdulmajid Nsekela amesema kuwa lengo la vituo vya biashara kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini ni kuboresha utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na hivyo kuchangia katika kuchochea ufanisi wa wafanyabiashara na kukuza uchumi. Hivyo wanataraji kuendelea kuwafikia wafanyabiashara popote walipo kwa huduma bora.
Aidha Afisa huyo wa Wateja Binafsi ameeleza kuwa katika mpango huo wanataraji kufanikisha malengo ya wateja wao ambao ni wafanyabiashara wakubwa, wa kati, wadogo sambamba na wakulima kwa kuboresha biashara ya kilimo.
Pia Bw. Nsekela amefahamisha kuwa pamoja na kufanya shughuli za kibenki, NMB pia inachangia shughuli za kijamii katika kuchangia maendeleo na wanatenga pato lao la mwaka kama mchango wao katika sekta ya afya na elimu ikiwa na lengo la kuiunga mkono Serikali ambapo wanatenga asilimia moja katika pato la mwaka kufanya shughuli hizo. 
Afisa huyo wa NMB amewataka wateja wa kati kuchangamkia fursa hiyo ambayo inawapa nafasi wafanyabiashara kupanda kutoka daraja moja kwenda lingine kulingana na ufanisi wa vituo vya biashara na elimu ya kifedha watakayopatiwa na NMB. 
Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi wa kituo cha biashara cha NMB mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abbas Kandoro amewataka wafanyabiasha na wakazi wa Mkoa huo kutumia fursa za kibenki ambazo zinatolewa ili kufikia malengo yao ya kibiashara.
Mh. Kandoro amefahamisha kuwa kabla ya kuchukua mkopo wanatakiwa kufanya tathmini na kujua biashara gani wanaweza kufanya na kuweza kufanya marejesho ya benki.
Pia Mh. Kandoro aliwataka viongozi wa benki ya NMB kuangalia suala la riba katika mikopo wanayotoa kwa vile wananchi wengi wanaogopa kukopa kutokana na baadhi ya mabenki nchini kutoza riba kubwa jambo linalowawia vigumu wafanyabiasha wadogo kujenga kasumba ya kuhofia mikopo kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi na kupanua wigo wa biashara zao. 
Benki ya NMB pia imejikita kwenye shughuli za kilimo kwa kuwezesha urahisi wa upatikanaji wa pembejeo ambapo hivi karibuni wameanzisha mpango wa kuwapatia wateja wake matrekta kwa gharama nafuu baada ya kuingia mkataba na kampuni ya Jebiz ambao ni wasambazaji wa matrekta.
Benki ya NMB ina matawi 175, Mashin za kutoa pesa (ATM) zaidi ya 600 na Mawakala ambao wanarahisisha shughuli za kibenki zaidi ya 450 pia wamejiunga na mitandao ya simu yanayotoa huduma za kifedha kwa njia ya simu. 
Kwa upande wa mikopo Mkuu wa Kitengo cha Biashara Bw. James Meitaron ameeleza utaratibu mzima wa utoaji wa mikopo kwamba kiwango ambacho wanaanzia kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ni kuanzia Shilingi milioni moja hadi milioni thelathini (milioni 30) mkopo ambao unapatikana ndani ya siku mbili na kuwa benki hiyo imempa mamlaka Meneja wa tawi kufanikisha mikopo ya kiwango hicho.
Kama biashara yako imeanza kukua, kituo cha biashara ambapo kwa Mbeya kipo NMB Mwanjelwa kinatoa mkopo kuanzia milioni 30 hadi bilioni 2.
Meitaron amesema kuwa riba ya mikopo kwa benki hiyo haizidi asilimia 23 kwa mwaka na kadiri unavyolipa mkopo riba inapungua mpaka kufikia asilimia 18 kulingana na mkopo uliokopa.