BENKI ya NMB imetoa elimu ya masuala ya kibenki na umuhimu wa kujijengea utamaduni wa uwekaji akiba kwa wanafunzi na baadhi ya wazazi wa Shule ya Msingi Wailes iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam. Akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Wailes walioshiriki mafunzo hayo ya kifedha, Ofisa wa Benki ya NMB Tawi la Temeke, Latifa Ayoub Dadah alisema NMB inaendelea kutoa elimu ya masuala ya kifedha ikiwa ni pamoja na kujifunza mbinu za kuweka akiba kwa ajili ya maisha ya baadae.
Alisema elimu hiyo inatolewa kupitia Programu maalum ya Wajibu ambayo hutoa fursa kwa watoto, vijana na wazazi kujifunza masuala ya kifedha ili kumjengea mtoto utamaduni wa kujiwekea akiba, elimu ambayo watoto wengi hawapati fursa ya kujifunza.
Akizungumza katika mafunzo hayo, alisema vijana wengi wamekuwa hawana utaratibu wa kujiweka akiba tangu wadogo hivyo NMB kupitia programu ya Wajibu inaendelea kutoa elimu kwa watoto, vijana pamoja na wazazi wao kuelewa umuhimu wa kujiwekea akiba ya fedha kupitia akaunti mbali mbali za benki hiyo, kama vile Mtoto Account, Chipukizi Account na Mwanachuo Account.
NMB katika ziara hiyo ambapo ilikuwa imeongozana na wachezaji wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Azam kupitia kituo chao cha michezo, mbali na anafunzi na wazazi kupata elimu ya masuala ya kifedha na uwekaji akiba kwa manufaa ya baadaye, wachezaji wa Azam walicheza mpira na wanafunzi hao pamoja na kugawa zawadi mbalimbali toka NMB na kampuni ya Azam.
Akifafanua zaidi, Bi. Latifa alisema elimu hiyo ni mwendelezo wa programu ya wajibu ambapo NMB imekuwa akizunguka katika shule mbalimbali za msingi na sekondari nchi nzima huku ikitoa elimu ya kifedha na masuala mazima ya uwekaji akiba. Alisema elimu hiyo itawasaidia watoto na vijana kufanya matumizi mazuri ya fedha kwa sasa na baadae, elimu ambayo wengi wameikosa. Alisema elimu hiyo ambayo imepokelewa vizuri kwa wanafunzi na wazazi ambao wameshiriki itaendelea kutolewa na benki hiyo hivyo kuwashauri wazazi na vijana kufungua akaunti mbalimbali ya NMB kulingana na maitaji yao ili waweze kunufaika.
“…Mwitikio kwa waliopata fursa ya kushiriki katika mafunzo haya ni mzuri kwa kwli hasa katika wilaya yetu ya Temeke, tumekuwa tukipokea watoto mbalimbali wakija kufungua akaunti jambo ambalo linaonesha wamevutiwa na elimu hii,” alisema ofisa huyo wa Benki ya NMB Tawi la Temeke.
Naye Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Msingi Wailes, Zabibu Wasia aliishukuru Benki ya NMB kwa kutoa mafunzo hayo kwa wanafunzi pamoja na baadhi ya wazazi/walezi wa shule hiyo na kuahidi kuendelea kuwa mabalozi kueneza elimu hiyo kwa wengine kutokana na umuhimu wake. “..Tunaishukuru sana NMB kwa kuamua kuleta elimu hiyo kwa wanafunzi na wazazi wa Wailes tunaamini hii ni fursa ya kipekee kwetu maana shule za msingi Dar es Salaam zipo nyingi lakini umeona muanze na sisi…tunashukuru sana kwa kutupendelea,” alisema Bi. Wasia.
Mbali na elimu hiyo NMB ilitoa mipira miwili kama zawadi kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Wailes, yaani mpira wa miguu kwa wanafunzi wa kiume na mpira wa pete kwa wanafunzi wa kike.