BENKI ya NMB imesisitiza kuwa huduma ya ‘Trade Fainance’ inayotolewa na benki hiyo inatarajiwa kuchochea ukuaji wa biashara ndani na nje ya nchi kwa Wafanyabiashara. Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kwenye semina, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bi. Ineke Bussemaker alisema huduma hiyo imewalenga wateja muhimu katika makundi yote ya wafanyabiashara wa kati na wakubwa ili kuzikuza biashara zao.
Alisema huduma ya ‘Trade Finance’ ni muhimu kwa biashara za ndani ya nchi na kimataifa, na Benki ya NMB imeiweka kuhakikisha inasaidia kukuza biashara zao. “Kwa lengo la Serikali ya Awamu ya Tano, kujenga uchumi wa viwanda kuna kila sababu ya Benki kubwa kama NMB kusaidia kukuza masoko kupitia huduma yake ya ‘Trade Finance’,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Bi. Bussemaker alipokuwa akifungua semina hiyo kwa wanahabari.
Aidha alifafanua kuwa, lengo la kampeni ya huduma ya NMB Trade Finance ni kuhakikisha inaonesha uhimara na ubora wa huduma yenyewe kibiashara na kuitangaza kwa wafanyabiashara, huku ikibainisha ilivyo msaada kwa bidhaa na huduma mbalimbali za wafanyabiashara ndani na nje ya nchi.