BENKI ya NMB imedhamini mkutano mkuu wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika kwa siku moja ya Aprili 4, 2017 mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na wahariri wa vyombo mbalimbali nchini ambao ni wanachama wa TEF.
Akizungumza katika uzinduzi wa mkutano huo, Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali, Richard Makungwa alisema NMB inathamini mchango wa waandishi wa habari nchini na imekuwa ikishikiana nao kwa muda mrefu hivyo kudhamini mkutano huo ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano ulipo baina ya NMB na waandishi wa habari.
“Kwa niaba ya uongozi wa Benki ya NMB, napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa kwa kutambua kuwa NMB ni benki iliyo karibu na jamii yote ya Watanzania na kugusa mahitaji ya kila jamii ya watanzania wa kila kada.
“Waandishi wa habari kwa NMB ni wadau muhimu sana kwani mafanikio ya NMB mpaka kufikia hapa kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na vyombo vya habari. Hivyo tunafarijika na sisi kushikiriana nanyi kwenye shughuli zinazowagusa ninyi moja kwa moja,” alisema Makungwa na kuongeza.
“Kwa NMB, huu ni mkutano muhimu sana na maazimio mtakayoyafikia, yatakuwa yenye tija huku mkiweka mbele uzalendo wan chi yetu. Mkiwa mnaendelea na mkutano huu, tambueni kuwa tunawathamini sana na kazi zenu tunazithamini sana.”
Udhamini wa NMB kwa mkutano mkuu wa mwaka wa TEF una thamani ya milioni 20 na hiyo siyo mara ya kwanza kwani hata mwaka jana ilidhamini mkutano wa TEF, mkutano mkuu wa mwaka wa TBN, mkutano wa TAJATI na pia NMB kuwezesha kutolewa kwa tuzo za uandishi mahiri kwa kushirikiana na MCT.