NMB kutoa mikopo kwa wajasiriamali

Na Mwandishi Wetu, Iringa

MUUNGANO wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) umefanikiwa kuwaunganisha wajasiriamali mkoani Iringa na Benki ya NMB mkoani humo, ili kuwasaidia kujipatia mafaniko zaidi katika kilimo.

Akizungumza na wajasiriamali hao, Mratibu wa MUVI mkoa huo, Wilma Mwaikambo Mtui (pichani juu), amesema changamoto kubwa inayowakabili wakulima wengi ni upatikanaji wa mbegu pamoja na pembejeo za kilimo, hivyo kitendo cha kuwanganisha na benki hiyo kutawasaidia wakulima kupata mikopo kwa ajili ya kununulia mbegu na pembejeo kadhaa za kilimo.

Naye Mwakilishi wa NMB Kanda ya Kusini, Roger Shipela ameeleza kuwa benki hiyo imeamua kujikita katika kilimo ili kuwasaidia wakulima kuimarisha vyama vyao na vikundi vya ushirika, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa vyama hivyo kupitia mfuko wa maendeleo ya kilimo yaani ‘NMB Foundation for Agriculture Development’.

Hata hivyo, Shipela amebainisha kuwa benki hiyo itatoa mikopo kwa vikundi vilivyo sajiliwa kwa kuwasiliana na uongozi wa MUVI ili kujua aina ya mkopo utakao tolewa kwa wajasiriamali hao. Alisema tayari benki hiyo imetoa mikopo kwa wakulima 15 wa alizeti, ikiwa ni pamoja na kuwapatia wakulima hao elimu kuhusina na mikopo hiyo.

Katika hatua nyingine Ofisa Habari wa MUVI, Mkoa wa Iringa William Macha, ameipongeza benki hiyo kwa juhudi za kuwasaidia wakulima na kuongeza kuwa kupitia mfuko huo wakulima watakuwa na uhakika kiuzalishaji kwani changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili ni ukosefu wa mitaji pamoja na masoko.

“Wajasiriamali wakipewa mikopo wataongeza kiwango cha uzalishaji, kwa kulima maeneo makubwa zaidi na kutumia mbegu bora na za kisasa, hivyo watapata mavuno yatakayokidhi soko la ushindani,” alisema Macha.