Na Mwandishi Wetu
BARA la Afrika ikiwemo Tanzania limeshakumbwa na matukio ya uhaba wa chakula, uliosababisha watu wengi kupoteza maisha hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara na Ukanda wa Sahel eneo la Afrika Magharibi.
Hali hiyo imekuwa moja ya changamoto kubwa inazozikabili Serikali za mataifa hayo ambapo yanapambana kuitatua ili kila mwananchi barani Afrika aweze kufurahia kukua kwa uchumi katika taifa lake.
Akitoa hotuba wakati akizindua rasmi Ripoti ya Maendeleo ya Afrika 2012 jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene (MB) amesema kwa muda mrefu sura ya eneo la nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara imekuwa ni ya njaa ya kukithiri, ambapo zaidi ya mtu mmoja katika kila waafrika wane wana tatizo la upungufu wa lishe.
Amesema ripoti hiyo inaonesha kuwa pamoja na ukweli kwamba baadhi ya nchi zinazokuwa kwa kasi kiuchumi katika kipindi cha miaka kumi ziko Afrika, lakini bado hali ya maisha ya waafrika ni duni.
Awali Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa UNDP nchini Tanzania Dk. Alberic Kacou alisema bara la Afrika limejaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba, maji ya kutosha na hali nzuri ya hewa kwa kukuzia mazao, lakini swali la kujiuliza ni kwanini bado kuna uhaba wa chakula.
Hata hivyo Dk. Kacou ametoa matumaini kuwa bara la Afrika bado lina uwezo wa kujijengea mazingira ya kuwa na akiba ya kutosha ya chakula kwa kipindi kijacho. Ripoti hii ya Kwanza ya Maendeleo ya Afrika inasema kwamba ongezeko endelevu katika uzalishaji kwenye kilimo kunalinda haki ya chakula na uwezo wa watu kupata chakula.