Na Mwandishi Wetu
OFISI ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inashiriki Maonesho ya 39 ya Biashara Kimataifa ikiwa na lengo la kuwasaidia wananchi mbalimbali kujua hatua zilizofikia vitambulisho vyao kwa ambao hawajapata na taarifa nyingine za taasisi hiyo muhimu.
Akizungumza na mtandao huu Ofisa Habari Mkuu Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Rose Mdami alisema moja ya shughuli wanazozifanya ndani ya Maonesho ya 39 ya Biashara Kimataifa maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam ni kuwasaidia wananchi kupata taarifa mbalimbali juu ya hatua zilizofikiwa kwa vitambulisho vyao.
“Moja ya shughuli tunazozifanya hapa sabasaba ni kuweza kuwasaidia wananchi kujua hatua zilizofikia vitambulisho vyao kwa ambao hawajapata, tunaangalia moja kwa moja kwenye mamlaka kuu inayoifadhi kumbukumbu na kuweza kujua kutambulisho kipo hatua gani,” alisema Bi. Mdami.
Alisema kuwa wanapofuatilia kuwa kuna tatizo lolote kwa mteja wao humjulisha mwananchi husika na kumuelekeza jinsi ya kukipata kitambulisho chake. “…Kikubwa ambacho tumesaidia hadi sasa hapa Sabasaba ni wananchi wamejitokeza na kujua taarifa za vitambulisho vyao…NIDA tupo kukuhudumia karibu ndani ya banda letu lipo ndani ya banda la Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) pia tunatoa msaada wa kupata taarifa mbalimbali kama kujua umuhimu wa vitambulisho, mfumo mzima wa usajili pamoja na kujua namna vitambulisho vitakavyotumika, alisisitiza Ofisa Habari huyo Mkuu wa NIDA.