Mtafiti wa kilimo kutoka taasisi ya Utafiti Kilimo Naliendele Festo Masisila akiwaeleza wakulima Thomas Mihambo (katikati) na Zuhura Nalipa (kulia) kutoka mtaa wa Mbawala Chini kata ya Naliendele mkoani Mtwara namna bora ya kulima zao la mhogo ikiwemo aina ya Kiroba, Pwani, Kizimbani, Makutupora, Dodoma, Mkumba na Mkuranga 1 inayostawi vizuri mkoani Mtwara wakati wa Maonesho ya Nane Nane kitaifa yanayoendelea katika uwanja wa Ngongo Mkoani Lindi.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka maofisa wa Serikali kuacha kabisa tabia ya kuwakopa wakulima masikini nchini kwa ujanjaujanja kwa kusingizia kuwa hawana fedha ya fidia mali zao ili kupisha ujenzi wa miradi mbali mbali ya Serikali. “Nimepata kulisema hili lakini nataka kulirudia tena, Serikali haiwezi kuendelea kuwakopa wakulima masikini kwa visingizio kuwa haina wala haijapata fedha za kufidia mali za wananchi kupisha miradi ya Serikali. Ni jambo la aibu kabisa kwa Serikali kuwakopa wakulima masikini,” amesema Rais Kikwete “Serikali hii haiwezi kufidiwa na masikini. Mnavunja nyumba za watu, mnaangusha minazi yao, mnakata miembe yao kwa kuwaambia kuwa hamna fedha za kuwalipa fidia ili kupisha miradi ya maendeleo ama kuwa fedha hizo zimechelewa. Ni aibu kwa Serikali kuwakopa masikini. Hata mimi ningejua kuwa mnataka kupitisha mradi bila kunifidia ningekataa kuwaruhusu kupitisha mabomba ya mradi shambani kwangu,” amesema Rais Kikwete. Rais alikuwa anazungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa mradi mkubwa wa maji katika eneo la Ng’apa, nje kidogo ya mji wa Lindi, ambako Rais amelalamikiwa na maofisa wa Serikali kuwa mradi huo ulichelewa kuanza kwa sababu baadhi ya watu waligoma mabomba ya mradi yasipitishwe kwenye maeneo na mashamba yao kwa sababu walikuwa hawajalipwa fidia. “Haya ni mawazo ya ovyo ovyo sana kwa maofisa wa Serikali kwamba mnaweza kuharibu mali za watu bila kuwalipa fidia. Ni aibu kubwa. Achaneni na mawazo haya. Badala ya kuwasaidia wakulima na wananchi masikini tunawalazimisha kupitisha nguzo za umeme ama mabomba ya maji kwenye mashamba yao bila kuwalipa fidia,” alisema Rais Kikwete na kuongeza: “Hakuna mradi unaoandaliwa bila kutilia maanani fidia ya watu. Pangeni mambo yenu vizuri siyo kudhulumu watu. Watu hawa ni masikini . Hata kama nyumba zao ni za makuti, hata kama ana mnazi mmoja ama mwembe mmoja bado ni mali yake anayo haki ya kunufaika nayo. Hatuwezi kuikata bila kumlipa fidia. Hili naomba lisirudiwe, popote nchini. Ni marufuku kwa Serikali kusaidiwa na masikini. Serikali haiwezi kufanya hivyo. Hii ni changamoto ya aibu.” Mradi wa maji wa Ng’apa unalenga kuchimba visima 10 kwa ajili ya kuwaongezea huduma ya maji safi na salama wakazi wa mji wa Lindi na baadhi ya vitongoji vyake ambao kwa sasa wanapata kiasi cha lita milioni 2,466 kwa siku. Mradi huo utaongeza kiasi cha lita milioni 7,500 za maji kwa ajili ya wakazi 82,000 wa maeneo hayo. Mradi huo ulioanza kujengwa Machi 18, mwaka juzi, 2013 lakini kwa sababu mbali mbali mradi huo umekuwa unacheleweshwa kumalizika. Mradi huo ulikuwa ujengwe kwa miezi 24 na umalizike Machi mwaka huu lakini inakadiriwa kuwa sasa utamalizika mwezi ujao. Mradi huo wa Ng’apa unaojengwa kilomita 12 kutoka mjini Lindi unajengwa kwa kiasi cha Euro milioni 11.6 na unagharimiwa
kwa pamoja na Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Ujerumani kupitia shirika lake la misaada ya maendeleo ya kimataifa la KFW chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Milenia. EU unagharimia mradi huo kwa asilimia 85 na Serikali ya Ujerumani kwa asilimia 15. Mradi huo wa maji wa Ng’apa ni moja ya miradi mitano inayogharimiwa kwa pamoja na EU na Serikali ya Ujerumani katika Tanzania. Miradi mingine iko katika miji ya Babati, Kigoma, Sumbawanga na Mtwara.