Maafa makubwa Dar, haijawahi tokea; Watu, nyumba zasombwa na mafuriko

Hata kama hutaki kuogelea utalazimika kufanya hivyo ili kujinusuru.

Baadhi ya wananchi wakiangalia Daraja la Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani likiwa limefunikwa na maji ya mvua leo.

Ni mafuriko magari yakipita kwa shida eneo la Sinza daraja la Shekilango

Baadhi ya nyumba zikiwa zimefunikwa na maji eneo la Daraja la Jangwani

Na Joachim Mushi

MVUA kubwa imeendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kusababisha maafa makubwa. Taarifa zinaeleza watu zaidi ya nane wanahofiwa kufa na uharibifu mkubwa wa mali za wananchi na miundombinu (madaraja) baada ya mafuriko makubwa kuyakumba maeneo ya mabonde ya Kigogo, Tandale, Tabata na Kiwalani jijini Dar es Salaam.

Taarifa zaidi zinasema huenda idadi ya watu waliopoteza maisha ikaongezeka kutokana na hali halisi iliyotokea. Baadhi ya barabara kama ile ya Morogoro kupitia daraja la Jangwani, Kawawa eneo la Kigogo, Mandela eneo la Relini, Ali Hassan Mwinyi eneo la Daraja la Sarenda, Daraja la Shekilango-Sinza zililazimika kufungwa kwa saa kadhaa kutokana na madaraja na vipande vya barabara kufunikwa na maji kabisa.

Baadhi ya familia zikiangalia makazi yao yakivamiwa na maji ya mafuriko jijini Dar es Salaam leo eneo la Kigogo


Maji mengi yaliyokuwa yakiporomoka yalilizifunika barabara na kupita juu ya madaraja ya barabara hizi hivyo magari na wananchi kushindwa kupita. Nyumba nyingi zimebomolewa na maji na vitu kupelekwa na maji hasa maeneo ya Kigogo Sambusa, Kigogo Post, Jangwani na Bonde la Mto Msimbazi.

Akizungumza na dev.kisakuzi.com leo jijini, Diwani wa Kigogo, Richard Chengula amesema mafuriko hayo yameleta maafa makubwa kwani baadhi ya wakazi eneo lake wanahofiwa kupoteza maisha (japokuwa amedai haijathibitika) huku mali nyingi zikiharibiwa na kupelekwa na maji.

Mwandishi wa dev.kisakuzi.com alishuhudia nyumba zikiwa zimebomolewa, zimezingirwa na mafuriko, zingine kufunikwa na maji kabisa maeneo ya Kigogo Darajani, Bonde la Msimbazi, Vingunguti, Kiwalani, Tabata Kisiwani na Relini.

Kituo cha daladala eneo la Jangwani Barabara ya Morogoro vikiwa vimejaa maji ya mafuriko.


Akizungumza na vyombo vya habari Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA), Dk. Agness Kijazi leo amesema mvua zilizonyesha leo ni kubwa na hazijawahi kutokea tangu mwaka 1954. Amesema mvua ya leo pekee imefikia kipimo cha milimita 156.4, huku ile ya jana ikifikia kipimo cha milimita 60.

Dk. Kijazi ameongeza kuwa kwa siku mbili yaani jana na leo mvua zilizonyesha Dar es Salaam zimefikia kipimo cha milimita 216.4 ikiwa ni kipimo kikubwa ambacho hakijawahi kutokea miaka mingi iliyopita na kuwataka wananchi waendelee kuwa na tahadhari kwani mvua itaendelea tena kesho.

Hata hivyo amesema utabiri wao unaonesha mvua hizo za msimu wa vuli zilizoanza kunyesha tangu Novemba 2011 zitaendelea hadi mwezi Aprili 2012.

Tayari Serikali imetenga maeneo maalumu ya kuwahifadhi waathirika wa maafa hayo ya mvua katika vituo vilivyo jirani na maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick amesema jumla ya watu nane wamefariki dunia, ambapo maiti sita zimeokotwa Wilaya ya Kinondoni, huku maiti moja moja zikiokotwa wilaya za Ilala na Temeke.

Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kuondoka mabondeni na kuacha kupuuzia maelekezo ya viongozi wa Serikali ambapo wamekuwa wakitoa kauli za kuwataka wanaoishi mabondeni kuhama maeneo hayo kutokana na msimu wa mvua za vuli kuanza.

Shughuli za kazi baadhi ya maofisi leo zimelazimika kufungwa baada ya majengo kadhaa kujaa maji na watu kushindwa kuingia wala kutoka katika majengo hayo. Vikosi vya uokoaji vilifanikiwa kuwaokoa baadhi ya wananchi katika ofisi hizo hasa za UNDP jijini Dar es Salaam na zile za makampuni na watu binafsi maeneo kadhaa.

Baadhi ya wakazi wa eneo la Daraja la Barabara ya Shekilango, Sinza-Kamanyola wakiangalia maji yaliyofurika kwenye mitaa ya eneo hilo leo.


Baadhi ya wananchi walilazimika kujiokoa kwa kuogelea kwenye maji machafu ambayo yalikuwa yakiporomoka na kupita katika mifereji mikubwa ya maji taka na Mto Msimbazi wa jijini Dar es Salaam uliopita maeneo kadhaa mjini hapa. Ukubwa wa athari haujaweza kujulikana mara moja.