Baadhi ya Wanamuziki wa Kundi la 5 Star waliojeruhiwa katika ajali iliyotokea juzi maeneo ya Mikumi Morogoro, wakiwa kwenye Ukumbi wa Ikweta Gril, baada ya kuwasili wakitokea Hospitali ya Morogoro jana. Picha na Mpigapicha Wetu
NI HUZUNI, ndivyo unavyoweza kuzungumzia ajali mbaya iliyochukua maisha ya wanamuziki 13 wa kundi la taarabu la Five Stars.
Ajali hiyo mbaya na pengine kubwa tangu kuanza kwa mwaka huu, ilitokea juzi usiku eneo la Doma lililopo ndani ya hifadhi ya Wanyamapori Mikumi.
Mbali ya kupoteza maisha kwa wanamuziki hao, pia ajali hiyo ilijeruhi wanamuziki wengine 12.
Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro Adolphina Chialo alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwataja waliofariki kuwa ni Issa Kijoti, Nassoro Madenge, Omary Hashim,Hassan Ngereza, na Husna Mapande.
Wengine ni Hamisa Musa,Tizo Mpunda, Rama Kinyoya, Jumanne maarufu Kasheba, Shjebe Juma, Omary Tall, Haji Mzamila, pamoja na wengine waliofahamika kwa jina mojamoja ambao ni Haji na Maimuna na maiti zilipelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya mkoa wa Morogoro kabla ya ndugu na jamaa kufika kuzichukua jana mchana.
Kamanda Adolphina aliwataja majeruhi ni Rajabu Kondo(24), Ally Juma(25), Suzan Benedict (32),Mwanahawa Ally (55), Zena Mohamed(27), Salum Jabir(31),Samina Rajab (22) na Mwanahawa Hamisi(2)
Wengine ni Msafiri Musa(22), Shabani Azizi(41) Issa Hamis pamoja na Mwanzani Said (19).
Alisema majeruhi hao walikuwa wakiendelea na matibabu katika hospitali hiyo ya Mkoa ambayo wote walilazwa hapo na wanaendelea vizuri isipokuwa Mwadhaani Said ambaye bado hali yake ni mbaya.
Inaelezwa bado chanzo cha ajali hakijafahamika ingawa inadhaniwa kuwa ni mwendo kasi wa dereva wa gari la wanamuziki hao ambalo ni T 351 BGE Toyota Costa lililokuwa likitokea Kyela Mkoani Mbeya kuja Dar es salaam.
Hata hivyo alisema dereva wa gari hilo bado hajafahamika jina kwani alikimbia baada ya kutokea kwa ajali hiyo.
Wakizungumza na Mtanzania katika hospitalini hapo, baadhi ya wanamuziki walionusurika, Zena Mohamed, Mwanahawa Ally, Mwanahamisi Hamisi, Issa Kamongo na Rajabu Kondo walisema dereva wao alikuwa akienda kasi na aliendesha bila kuchukua tahadhari za barabarani.
Walisema wakiwa kwenye gari waliona mbele lori lilokuwa limepakia mbao likiwa limesimama bila kuonyesha alama zozote za tahadhari na dereva wao alitaka kulipita lori hilo na ghafla mbele kukawa na lori jingine linakuja na hivyo kwenda kuligonga lori lilokuwa limesimama.
“Tulishtuka ghafla na kuona dereva wetu akirikaribia lori lililokuwa limesimama bila kuonyesha ishara ya kama limeharibika au vipi, tukawa tumelikaribia mno na ndipo dereva wetu aliamua kulipita ghafla kule kukawa na lori lingine linakuja.
“Kuona vile ikabidi arudi na ndipo tulipolivaa lile lori lililokuwa limesimama na lile lori lilokuwa linakuja lilitugonga ubavuni na gari yetu kupinduka.
Baada ya hapo sikujua kilichoendelea na ndio nimejikuta niko hapa hospitali na kuambiwa wenzetu wamekufa, inauma sana,” alisema Mwanahawa.
Kutoka na vifo hivyo, Mtanzania liliamua kuzunguka kumbi mbalimbali ambazo kundi hilo lilikuwa likifanya shoo zake na kuzungumza na mashabiki wao na wale wa taarabu kwa ujumla ambapo wengi walionekana kuchanganyikiwa na kutoamini habari hizo.
“Mimi siamini hata kidogo, kwanza nilianza kupata habari jana usiku kati ya saa 3.00 na saa 4.00, sikuamini kwasababu kila mmoja alikuwa anasema kivyake.
“Wapo waliokuwa wanazusha mara Jahazi, mara New Modern Taarabu hivyo nilishindwa kuamini lipi ni lipi hadi asubuhi nilipopata taarifa katika luninga na baadhi ya vituo vya radio, lakini bado siamini hadi miili yao itakapokuja Dar es Salaam,” alisema Aisha Mwange mkazi wa Lango la jiji. Magomeni.
Kutokana na vifo hivyo, maeneo kadhaa ya jiji la Dar es Salaam na viunga vyake yalizizima kwani kila ulipokuwa unapita kulikuwa na vikundi vya watu ambao wanazungumzia tukio hilo huku wakikumbushana kwamba ndilo kundi lililotikisa na vibao kadhaa kama kile cha Noma na Mchumu ambavyo ndivyo vinafahamika vema.
Huku maeneo mengine kama Kariakoo, Magomeni na Mbagala ambako Mtanzania ilitembelea na kuzungumza na mashabiki wa kundi hilo ambao wako wengi maeneo hayo kutokana na kutoa burudani mara kwa mara karibu wote walikuwa na simanzi na baadhi ya maeneo hayo kulikuwa kukipigwa nyimbo za kundi hilo.
Mtanzania inaungana na ndugu, jamaa na watanzania wote kwa ujumla katika kuomboleza msiba huu mzito katika tasnia hiyo ya taarabu na Mungu aiweke roho za marehemu mahali pema peponi, Amina.Watanzania tuliwapenda, ila Mungu kaipenda zaidi Five Stars Modern Taarabu.Soma makala ya kundi hilo
chanzo:gazeti la Mtanzania