MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya nchini (NHIF) leo umetoa elimu ya umuhimu wa viongozi wa Jumuiya ya Zawiyatul Qadiria kujiunga na mpango wa huduma za matibabu ya bima ya afya unaotolewa kwa makundi yenye malengo mbalimbali ujulikanao kama KIKOA.
Akizungumza wakati akifungua semina kwa viongozi hao Kaimu Mkurugenzi wa NHIF, Eugine Ngoti alisema mfuko huo umelenga kuhakikisha unaendelea kutoa huduma za afya kwa wigo mpana zaidi ndio maana wamekuja na mpango wa KIKOA unaowapatia fursa makundi/vikundi anuai vya jamii kunufaika na huduma za afya hata kama wamejiajiri wenyewe katika shughuli zao.
Alisema lengo la NHIF ni kuhakikisha huduma zao zinawafikia Watanzania wote huku kukiwa na utaratibu nafuu wa kuchangia na hatimaye makundi anuai kunufaika na huduma za afya zinazotolewa na shirika hilo. Alisema kwa sasa NHIF imefanikiwa kutoa huduma hiyo kwa asilimia 20 ya Watanzania wote huku uhamasishaji na elimu vikiendelea ili kuwafikia wengi zaidi.
Aidha aliwataka viongozi hao wa dini kupitia Jumuiya yao ya Zawiyatul Qadriya kuhakikisha wanawasaidia hata viongozi wasiokuwa na uwezo wa kuchangia wanapata fursa hiyo ili waweze kunufaika na huduma za afya kwa mpango rahisi wa kuchangia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Matengenezo wa viongozi wa Jumuiya ya Zawiyatul Qadiria, Alhaji Said Rashid Kilahama aliishukuru NHIF kwa kuanzisha mpango ambao unawawezesha makundi mbalimbali wakiwemo wanyonge kupata huduma za afya kwa utaratibu rahisi wa uchangiaji mdogo. Alisema utaratibu huo unawawezesha hata makundi ya wanyonge kujikuta wakinufaika na huduma za afya.
“…Wengi katika Jumuiya wengi hawamo katika utaratibu wa huduma za afya lakini naimani baada ya mafunzo haya na kutufumbua macho wengi tutajiunga na kuanza kunufaika moja kwa moja…ninachokifurahisha zaidi katika huduma zenu ni kitendo cha kuwajali hadi wanyonge…,” alisema alhaji Kilahama akizungumza katika semina hiyo.
Mpango wa KIKOA unawawezesha wanachama walio katika kikundi/ushirika halali unaofanya shughuli zinazokubalika kisheria kunufaika na huduma za matibabu kwa kuchangia shilingi 76,800 kwa kila mnufaika kwa kila mwaka na kupata matibabu, huku fedha hizo kukusanywa na viongozi wa kikundi/ushirika husika na kukabidhi NHIF moja kwa moja.