Na Joachim Mushi
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limeweka hadharani taarifa za madeni ya mpangaji wao Kibore Macho Mzee ambae hivi karibuni aliwatishia kwa bastola maofisa wa shirika hilo pamoja na kampuni inayokusanya madeni ya shirika walipomfuata kutaka kumtoa kwenye nyumba.
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utawala wa NHC, Raymond Mdolwa amesema mteja huyo aliyepanga Mtaa wa Jamhuri kiwanja namba 1620-23/129 anadaiwa na shirika hilo jumla ya sh. 1,538,848.60 ikiwa ni malimbikizo ya kodi tangu mwezi Machi 2011.
Alisema mara kadhaa ametumiwa taarifa na NHC aeleze kwanini hataki kulipa deni lake lakini hakutoa ushirikiano wowote, hivyo kung’ang’ania ndani ya nyumba ya shirika kwa miezi 13 bila kufanya malipo yoyote, jambo ambalo ni kinyume na mkataba wake.
“Inasikitisha kuona kwamba licha ya kupewa notisi ya kuvunja mkataba ya siku 30 kutoka Shirika la Nyumba la Taifa na notisi ya siku 14 toka kwa dalali wa kukusanya madeni bado alikataa sio kulipa deni lake tuu bali pia hakutoa maelezo yeyote ya ni kwanini hataki kulipa deni hilo,” alisema Mdolwa.
Ameongeza kuwa baada ya kushindikana waliamua kumuondoa kwa nguvu ndipo alipotumia bastola kwa kupiga hewani kuwatishia baadhi ya maofisa wa NHC, wafanyakazi toka kampuni ya kukusanya madeni na wanahabari ambao walikuwa eneo la tukio, hadi pale walipotaarifiwa polisi na kuja kumtia nguvuni.
Akizungumzia mafanikio ya zoezi la ukusanyaji madeni, Mdolwa alisema NHC imekusanya jumla ya sh. 2,594, 276,431.76 kwa kipindi cha kuanzia Oktoba hadi Desemba 2011.
“Zoezi hili limepata mafanikio makubwa tumekusanya jumla ya sh. 2,594, 276,431.76,…pesa hizi ni zile zilizotokana na malimbikizo ya madeni kwa wadaiwa wa muda mrefu…, wateja wa nyumbani pamoja na biashara tumekusanya jumla ya sh. 1,926,892,029.20, kutoka serikalini na taasisi zake zote tumekusanya jumla ya sh. 667,384, 402.50,” alisema Ofisa huyo wa NHC.
Aidha akifafanua zaidi alisema wakiwa wanaanza zoezi la ukusanyaji madeni taasisi za Serikali zilikuwa zinadaiwa jumla y ash bilioni 2.1 na tayari taasisi hizo zimeingia mikataba ya kulipa madeni yao kwa awamu.