Na Mwandishi Wetu, Arusha
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limezindua mauzo ya nyumba katika mradi wake mpya wa Levolosi, jijini hapa, mradi wenye nyumba 100 unaotarajiwa kukamilika Januari mwakani.
Aidha uzinduzi huo ni mfululizo wa uzinduzi wa miradi ya NHC ambao unalenga kutimiza malengo ya mkakati wa shirika kwa mika mitano wa kujenga nyumba 15,000 kote nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa shirika hilo David Shambwe, alisema kuwa ujenzi wa nyumba hizo ulianza Januari mwaka huu.
Alisema kuwa nyumba 30 hazitauzwa na badala yake zitatumika kuwahamishia watu ambao maeneo yao yatakuwa yamechukuliwa ili kupisha ujenzi wa nyumba za kisasa unaofanywa na shirika hilo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa kati ya nyumba hizo 15,000, nyumba 10,000 ni wka ajili ya wananchi wa kipato cha kati na cha juu na 5,000 kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini.
Aidha mradi huo upo katika eneo la Levolosi kwenye barabara ya kuelekea Ngarenaro na Nairobi karibu na Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC), mradi ambao lengo lake ni kuboresha maisha ya wanunuzi wa nyumba hizo kutokana na nyumba hizo kuwa karibu na katikati ya jiji ambapo huduma za kijamii hupatikana kwa urahisi zaidi.
Shambwe alifafanua kuwa mradi huo wa nyumba 100, hadi kukamilika kwake utakuwa umegharimu kiasi cha sh. bilioni (6) sita. Alisema shirika linawahamasisha na kuwakaribisha Watanzannia wote walio ndani na nje kufanya mawasiliano na makao makuu ya shirika, ofisi za mikoa, au kupitia barua pepe na kukamilisha taratibu mapema
kwa ajili ya kuweza kuingia kwenye mchakato ulio wazi wa manunuzi.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa gharama ya ardhi kuwa kuwba ni moja ya kikwazo kwa wananchi na kuzisihi halmashauri mbalimbali hapa nchini kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji au kuyagawa bure kwa shirika hilo ili liweze kujenga nyumba za gharama nafuu na kuwauzia wananchi