Newcastle, Arsenal watoka sare, Bolton yauwa, Leverpool yakwama

Mchezaji, Gervinho Kouassi

NEWCASTLE imetoka sare ya 0-0 na Arsenal katika mchezo uliokuwa na kasoro za hapa na pale. Katika mchezo huo mshambuliaji wa Arsenal kutoka Ivory Coast, Gervinho alioneshwa kadi nyekundu baada ya kushikana mashati na Joey Burton wa Newcastle.

Awali Burton alikanyagwa kwa makusudi na Alex Song, ingawa mwamuzi hakuona tukio hilo. Arsenal licha ya kujaribu kucheza mtindo wao wa ‘kuteleza’ walishindwa kuivunja ngome ya Newcastle. Wakicheza bila ya Cesc Fabregas na Samir Nasri, Arsenal walionekana kupata tabu kutengeneza nafasi.

Wakati huo huo mwingine mchezaji, Sebastian Larsson alifunga bao maridadi la kusawazisha na kufanikiwa kuipatia timu yake ya Sunderland pointi moja dhidi ya Liverpool katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Soka ya England.

Wenyeji Liverpool ilikuwa wapate bao mapema lakini mkwaju wa penalti uliopigwa na Luis Suarez ukapaa juu la lango la Sunderland. Suarez alisukumwa na mlinzi Kieran Richardson, lakini dakika chache baadae akarekebisha makosa na kufunga bao la kwanza kwa Liverpool baada ya kuunganisha kwa kichwa mkwaju uliochongwa na Charlie Adam.

Sunderland katika kipindi cha kwanza hawakuonekana tishio sana langoni mwa Liverpool, lakini katika dakika ya 57 Larson alipata nafasi ya kuunganisha mkwaju wa pembeni uliopigwa na Ahmed El Mohammedy na kuisawazishia timu yake kwa bao safi sana huku ngome ya Liverpool ikiwa inamuangalia tu bila kumkabili.

Matokeo hayo yamezifanya timu hizo zigawane pointi moja. Nayo QPR imeanza Ligi Kuu ya soka ya England kwa kupachikwa mabao manne huku Bolton ikiwafundisha soka katika mechi yao ya kwanza ya kufungua msimu wa Ligi Kuu ya England.

Timu hiyo ya QPR ikicheza katika uwanja wa nyumbani ilicheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini wakawa wanazorota kila muda ulivyokuwa ukiyoyoma.

Mabao hayo manne ya Bolton yalifungwa na Gary Cahill kwa mkwaju wa mbali kipindi cha kwanza, Danny Gabbidon mlinzi wa QPR akajifunga mwenyewe bao la pili na Ivan Klasnic akapachika bao la tatu.

Fabrice Muamba alikamilisha kitabu cha mabao kwa kufunga bao la nne, kabla ya mchezaji wa QPR kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Matokeo hayo yanaifanya Bolton kuanza ligi kwa kuongoza ikiwa na pointi 3 na mabao manne.

Wolverhampton Wanderers ikiwa ugenini imeshalazwa bao 1-0, ilijipapatua na kuweza kurejesha bao na hatimaye kufanikiwa kuilaza Blacburn mabao 2-1.

Blackburn Rovers walitangulia kufunga baada ya Jason Roberts kumtangulizia mpira Mauro Formica ambaye mkwaju wake wa chini ulimshinda mlinda mlango Wayne Hennessey.

Lakini Wolves ilijiuliza na kusawazisha bao lililofungwa na Steven Fletcher kwa kichwa kutokana na krosi iliyochongwa na Matt Jarvis. Stephen Ward aliipatia bao la ushindi Wolves kwa mkwaju wa juu baada ya Kevin Doyle kukosa mkwaju wa penalti.

Nayo timu mpya iliyopanda ligi msimu huu ya Norwich ilipigana kiume na kuweza kuilazimisha Wigan kutoka nayo sare ya kufungana bao 1-1, katika mechi ya kufungua msimu huu.

Wigan walikuwa wa kwanza kufunga bao katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Ben Watson kwa mkwaju wa penalti baada ya Ritchie de Laet kuangushwa na Franco di Santo.

Norwich walisawazisha wakati mpira ukielekea mapumziko kwa bao la Wes Hoolahan kutokana na makosa ya mlinda mlango Ali Al-Habsi.

Mechi nyingine ilikuwa ni kati ya Fulham waliowakaribisha Aston Villa, ambapo mechi hiyo haikushuhudia mabao, baada ya timu hizo kushindwa kufungana hadi dakika tisini za mchezo.