NEMC Yakifunga Kiwanda cha 21st Century

Moja ya mabwawa ya maji taka ya kiwanda cha nguo cha 21st Century

Moja ya mabwawa ya maji taka ya kiwanda cha nguo cha 21st Century

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KIWANDA cha nguo cha 21st Century kilichopo eneo la Kihonda Mkoani Morogoro kimefungiwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kutokana na kudaiwa kutiririsha maji taka ambayo yamekuwa yakichafua mazingira. Taarifa ya NEMC imekitaka kiwanda hicho kusimamisha shughuli zote za uzalishaji kuanzia Februari 20, 2015.

Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa NEMC, Dk. Robert Ntakamulenga akizungumza na vyombo vya habari leo mjini Dar es Salaam alisema mtambo wa kutibu majitaka wa kiwanda hicho hauna uwezo wa kuyatibu majitaka hayo kufikia viwango vya mazingira vinavyokubalika.

Dk. Ntakamulenga alisema majitaka ya kiwanda hicho yanachafua mazingira jambo ambalo linaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa jamii kutokana na maji kuwa na rangi nzito na kemikali anuai ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu na viumbe wengine eneo hilo.

“Tangu mwaka 2006 Baraza na kwa nyakati tofauti na mamlaka nyingine zikiwemo za dola, wametoa maelekezo na amri mbalimbali kwa uongozi wa kiwanda hicho ili kuboresha mfumo wake wa kutibu majitaka yatokayo kiwandani humo kabla ya kuyaruhusu kuingia katika mabwawa ya kutibu majitaka yaliyokuwa yakimilikiwa na shirikisho la viwanda vya ngozi(TLAI) ambao sasa haupo, lakini kiwanda hicho kimeendelea kukaidi maagizo na maelekezo hayo hadi sasa,” alisema.

Aidha aliongeza kuwa mabwawa ya kutibu majitaka yaliyokuwa yakimilikiwa na TLAI yalijengwa mahsusi kwa kutibu majitaka yatokanayo na viwanda vya ngozi na si majitaka yatokanayo na kiwanda cha nguo kwani majitaka yatokanayo na kiwanda cha nguo yana kemikali na tindikali ambayo inaharibu mfumo wa ufanyaji kazi wa mabwawa.

“…Majitaka hayo sasa yanapita tu bila kusafishwa au kutibiwa na kuingia mto Ngerengere ambao nao unamwaga maji yake katika Mto Ruvu ambao ni chanzo kikubwa cha maji kwa matumizi mbalimbali wakiwemo wakazi wa mikoa ya Pwani na Dar es salaam,” alisema Dk. Ntakamulenga.

Alibainisha kutokana na kiwanda hicho kushindwa kurekebisha hali hiyo licha ya maelekezo waliyopewa awali, Baraza linaamini kwamba kuendelea kufanya kazi kwa kiwanda hicho kutasababisha athari kubwa kwa mazingira na afya ya wananchi ambao kwa namna moja au nyingine wanatumia maji ya Mto Ngerengere.

“Hivyo kwa kutumia mamlaka lililopewa chini ya sheria ya Mazingira, Baraza linatoa amri ya kukifungia kiwanda hicho mpaka hapo kitakapotekeleza masharti yote yaliyotolewa na Baraza kikamilifu na Baraza kuridhika na utekelezaji huo,” alisema.

Pamoja na hayo amevitaka viwanda vyote nchini vinavyotumia nishati ya kuni kusitisha matumizi yao badala yake watumie nishati ya gesi, makaa yam awe na umeme. Dk. Ntakamulenga alisema kuwa Machi mosi mwaka huu wanaanza operesheni ya kukamata mifuko ya plastiki isiyokuwa na viwango ambapo wauzaji wote wa mifuko hiyo watatakiwa kujiandikisha NEMC kwa mujibu wa kanuni zitakazotolewa.