RAIS wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amesema kuwa Hayati Nelson Mandela anatarajiwa kuzikwa Desemba 15 ya Jumapili katika Kijiji cha Qunu Mkoa wa Eastern Cape, nchini Afrika Kusini. Rais Zuma ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya kiongozi huyo maarufu duniani, Mandela kufariki dunia. Wananchi wameendelea kujitokeza katika sehemu nyingi za Afrika Kusini wakiomboleza kifo cha kiongozi huyo.
Taarifa zinasema Mji wa Johannesburg umeendelea kuongezeka watu wakijitokeza kumkumbuka Mandela na kutoa salamu za rambirambi zao kwa ndugu, jamaa na marafiki. Mazishi ya kiongozi huyo maarufu ulimwenguni huenda yakabeba historia ya pekee ulimwenguni kutokana na kuyagusa mataifa mengi makubwa kwa pamoja huku yakioneshwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya viongozi.
Wakati hayo yakiendelea viongozi kutoka sehemu mbalimbali za dunia wameendelea kutuma rambirambi zao kufuatia kifo cha Mandela. Kifo cha Mandela kilitangazwa Alhamisi majira ya saa nne za usiku na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma; aliyesema kuwa Afrika Kusini inaomboleza kumpoteza kiongozi huyo waliyemuenzi sana kama mtoto wao, baba yao na kiongozi wa taifa hilo.
rais wa Afrika Kusini Zuma ametangaza siku 10 za maombolezo kwa Mandela aliyefariki Alhamisi akiwa na umri wa miaka 95. Maelfu ya watu wameweka maua nje ya makazi yake kuonesha mapenzi yao kwa Mandela. Ikulu ya Marekani kupitia Rais wake Barack Obama na mkewe Machelle wametangaza kwenda Afrika Kusini wiki ijayo kuungana na viongozi wengine wengi wa dunia, katika ibada ya kumuaga Nelson Mandela.
Katika msafara huo Obama ataambatana na watangulizi wake wake wawili, George W Bush na Bill Clinton, ambao pia watasindikizwa na wake zao. Rais Obama ataongoza ujumbe wa Marekani kwenye ibada ya kumkumbuka Mandela. Taarifa zinasema Mwili wa Mandela utawekwa katika jengo la serikali kwa muda wa siku tatu, kutoa fursa kwa wananchi wa Afrika Kusini kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi waliyempenda.
Baadaye mwili wake utasafirishwa kwenda Kijijini Qunu. Mayor wa jiji la Cape Town Patricia de Lille alisema katika ibada hiyo kuwa watu wa mji huo, weusi kwa weupe, wahidi na wenye damu mchanganyiko, wanaungana kwa mshikamano kumuenzi Nelson Mandela na kukumbuka mchango wake kwa nchi yao.
Kifo cha Mandela kimeiunganisha dunia kwa sasa kwani nchi kadhaa ulimwenguni zilitangaza maombolezo kwa kifo hicho huku mataifa makubwa kama Marekani, Ufaransa na Uingereza nakipeperusha bendera nusu mringoti. Baadhi ya nchi za Afrika nazo zilipepeza bendera nusu mringoti pamoja na makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa Mzee Mandela, ni miongoni mwa wengine kama Oliver Tambo, Govan Mbeki na wengine, waliojitolea maisha yao na ujana wao wote katika kupigania haki na kuikomboa Afrika Kusini. Walijivunia walichoamini na wakatekeleza. Sasa ni jukumu letu na wadogo wetu kuendeleza kazi ya Mandela.
Kwa upande wake Rais wa Malawi Joyce Banda, amesikika katika vyombo vya habari ulimwenguni akisema kuwa wakati kama huu, sote tumepata mshtuko. Sio kuwa hatukujua kitatokea, lakini ni huzuni kwa tulichopoteza. “…Ningependa kuelezea masikitiko yangu kwa kumpoteza kijana wa Afrika…Nelson Mandela kwasababu vita alivyopigana sio tu dhidi ya ubaguzi wa rangi bali ni vita dhidi ya unyanyasaji wa aina yoyote dhidi ya binadamu,” alisema Banda.
Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, “Kifo cha mandela. Huyu alikuwa mwakilishi wa utu duniani. Pia amekuwa chanzo cha matumaini kwa wengine wengi ambao wanakabiliana na unyanyasaji na kunyimwa haki, hata miaka yote hiyo baada ya kuwakomboa watu wake wenyewe. Katika ulimwengu uliogubikwa na migawanyiko, amekuwa mfano mwema wa utangamano na sioni uwezekano wa kupatikana mwingine kama yeye katika miaka mingi ijayo.” Taifa la India pia limetangaza siku tano za maombolezo kwa msiba wa Mandela.
Mandela alifariki nyumbani kwake mjini Johanesburg na alikuwa ameugua homa ya mapafu kwa muda mrefu hivi sasa.
-Vyanzo anuai duniani